Mathayo 6:16-24
Mathayo 6:16-24 NENO
“Mnapofunga, msiwe wenye huzuni kama wafanyavyo wanafiki. Maana wao hukunja nyuso zao ili kuwaonesha wengine kwamba wamefunga. Amin, amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao kamilifu. Lakini unapofunga, jipake mafuta kichwani na kunawa uso wako, ili kufunga kwako kusionekane na watu wengine ila Baba yako anayeketi mahali pa siri; naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako kwa wazi. “Msijiwekee hazina duniani, ambapo nondo na kutu huharibu, nao wezi huvunja na kuiba. Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wezi hawavunji na kuiba. Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa. “Jicho ni taa ya mwili. Kama jicho lako ni nyofu, mwili wako wote utajaa nuru. Lakini kama jicho lako ni ovu, mwili wako wote utajawa na giza. Hivyo basi, ikiwa nuru iliyo ndani yako ni giza, je, hilo ni giza nene aje! “Hakuna mtu awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.