Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 9:18-31

Mathayo 9:18-31 NEN

Yesu alipokuwa akiwaambia mambo haya, mara akaingia kiongozi wa sinagogi akapiga magoti mbele yake, akamwambia, “Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini njoo uweke mkono wako juu yake, naye atakuwa hai.” Yesu akaondoka akafuatana naye, nao wanafunzi wake pia wakaandamana naye. Wakati huo huo, mwanamke mmoja, ambaye alikuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, akaja nyuma ya Yesu, akagusa upindo wa vazi lake, kwa maana alisema moyoni mwake, “Kama nikigusa tu vazi lake, nitaponywa.” Yesu akageuka, naye alipomwona akamwambia, “Binti, jipe moyo mkuu, imani yako imekuponya.” Naye yule mwanamke akapona kuanzia saa ile ile. Yesu alipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi na kuwaona waombolezaji wakipiga filimbi za maombolezo na watu wengi wakipiga kelele, akawaambia, “Ondokeni! Kwa maana binti huyu hakufa, bali amelala.” Wakamcheka kwa dhihaka. Lakini watu walipokwisha kutolewa nje, akaingia mle ndani na kumshika yule binti mkono, naye akaamka. Habari hizi zikaenea katika maeneo yale yote. Yesu alipokuwa akiondoka mahali pale, vipofu wawili wakamfuata wakipiga kelele kwa nguvu na kusema, “Mwana wa Daudi, tuhurumie!” Alipoingia mle nyumbani wale vipofu wakamjia. Naye Yesu akawauliza, “Mnaamini kwamba ninaweza kufanya jambo hili?” Wakamjibu, “Ndiyo, Bwana.” Ndipo Yesu akagusa macho yao na kusema, “Iwe kwenu sawasawa na imani yenu.” Macho yao yakafunguka. Yesu akawaonya vikali, akisema, “Angalieni mtu yeyote asijue kuhusu jambo hili.” Lakini wao wakaenda na kueneza habari zake katika eneo lile lote.