Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 5

5
Isa amponya mtu mwenye pepo mchafu
(Mathayo 8:28-34; Luka 8:26-39)
1Isa na wanafunzi wake wakafika upande wa pili wa ziwa, wakaingia katika nchi ya Wagerasi. 2Isa alipotoka kwenye mashua, mara mtu mmoja mwenye pepo mchafu akatoka makaburini, akakutana naye. 3Mtu huyu aliishi makaburini, wala hakuna aliyeweza kumzuia hata kwa kumfunga minyororo. 4Kwa kuwa mara kwa mara alikuwa amefungwa minyororo mikononi na miguuni, lakini akaikata hiyo minyororo na kuzivunja zile pingu miguuni mwake. Hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa na nguvu za kumzuia. 5Usiku na mchana alikuwa makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikatakata kwa mawe.
6Alipomwona Isa kwa mbali, alimkimbilia, akapiga magoti mbele yake. 7Akapaza sauti kwa nguvu akisema, “Una nini nami, Isa, Mwana wa Mungu#5:7 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili. Aliye Juu Sana? Ninakusihi kwa jina la Mungu, usinitese!” 8Kwa kuwa Isa alikuwa amemwambia, “Mtoke mtu huyu, wewe pepo mchafu!”
9Isa akamuuliza, “Jina lako ni nani?”
Akamjibu, “Jina langu ni Legioni#5:9 maana yake Jeshi, kwa kuwa tuko wengi.” 10Akamsihi Isa sana asiwapeleke nje ya nchi ile.
11Palikuwa na kundi kubwa la nguruwe lililokuwa likilisha karibu kando ya kilima. 12Wale pepo wachafu wakamsihi Isa wakisema, “Tuamuru twende kwenye wale nguruwe. Turuhusu tuwaingie.” 13Basi Isa akawaruhusu, nao wale pepo wachafu wakatoka, wakawaingia hao nguruwe. Lile kundi lilikuwa na nguruwe wapatao elfu mbili, nao wote wakateremkia gengeni kwa kasi, nao wakatumbukia ziwani na kuzama.
14Wale watu waliokuwa wakichunga hao nguruwe wakakimbilia mjini na vijijini kueleza yaliyotukia. Watu wakaenda kuona hayo yaliyokuwa yametukia. 15Walipofika kwa Isa, wakamwona yule mtu aliyekuwa amepagawa na legioni ya pepo wachafu akiwa ameketi hapo, amevaa nguo na mwenye akili timamu. Wakaogopa. 16Wale walioyaona mambo hayo wakawaeleza watu wengine yaliyomtokea yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu, na habari za lile kundi la nguruwe pia. 17Basi watu wakaanza kumwomba Isa aondoke katika nchi yao.
18Isa alipokuwa anaingia kwenye mashua, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu akamsihi Isa waende pamoja. 19Isa hakumruhusu, bali alimwambia, “Nenda nyumbani kwa jamaa yako ukawaeleze mambo makuu aliyokutendea Mwenyezi Mungu, na jinsi alivyokuhurumia.” 20Yule mtu akaenda zake, akaanza kutangaza katika Dekapoli mambo makuu Isa aliyomtendea. Nao watu wote wakastaajabu.
Isa amponya mwanamke na kumfufua msichana
(Mathayo 9:18-26; Luka 8:40-56)
21Isa alipokwisha kuvuka tena na kufika ng’ambo, umati mkubwa wa watu wakamzunguka hapo kando ya bahari. 22Kisha mmoja wa viongozi wa sinagogi#5:22 Nyumba ya ibada na mafunzo. aliyeitwa Yairo akafika pale. Naye alipomwona Isa, akapiga magoti miguuni pake, 23akamsihi akisema, “Binti yangu mdogo ni mgonjwa mahututi. Tafadhali nakusihi, njoo uweke mikono yako juu yake ili apate kupona, naye ataishi.” 24Hivyo Isa akaenda pamoja naye.
Umati mkubwa wa watu wakamfuata, nao watu wakawa wanamsonga. 25Hapo palikuwa na mwanamke aliyekuwa amesumbuliwa na tatizo la kutokwa damu kwa miaka kumi na mbili. 26Mwanamke huyu alikuwa ameteseka sana kwa mikono ya matabibu wengi, na kutumia kila kitu alichokuwa nacho. Lakini badala ya kupona, hali yake ilizidi kuwa mbaya. 27Alikuwa amesikia habari za Isa, naye akaja kwa nyuma yake kwenye umati wa watu, akaligusa vazi lake, 28kwa maana alisema moyoni mwake, “Nikiligusa vazi lake tu, nitaponywa.” 29Mara kutoka damu kwake kukakoma, naye akajisikia mwilini mwake amepona kabisa.
30Ghafula Isa akatambua kuwa nguvu zimemtoka. Akageukia umati wa watu na kuuliza, “Ni nani aliyegusa mavazi yangu?”
31Wanafunzi wake wakamjibu, “Unaona jinsi watu wanavyokusonga. Wawezaje kuuliza, ‘Ni nani aliyenigusa?’ ”
32Lakini Isa akaangalia pande zote ili aone ni nani aliyemgusa. 33Yule mwanamke, akijua kilichomtokea, akaja, akaanguka miguuni pake akitetemeka kwa hofu, akamweleza ukweli wote. 34Isa akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.”
35Alipokuwa bado anaongea, watu wakafika kutoka nyumbani mwa Yairo. Wakamwambia, “Binti yako amekufa. Kwa nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?”
36Aliposikia hayo waliyosema, Isa akamwambia huyo kiongozi wa sinagogi, “Usiogope. Amini tu.”
37Hakumruhusu mtu yeyote amfuate isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, nduguye Yakobo. 38Walipofika nyumbani mwa yule kiongozi wa sinagogi, Isa akaona ghasia, watu wakilia na kuomboleza kwa sauti kubwa. 39Alipokwisha kuingia ndani, akawaambia, “Kwa nini mnafanya ghasia na kulia? Mtoto hajafa, bali amelala tu.” 40Wale watu wakamcheka.
Baada ya kuwafukuza wote nje, Isa akaenda na baba na mama wa yule mtoto, pamoja na wale wanafunzi aliokuwa nao, wakaingia ndani hadi pale alipokuwa mtoto yule. 41Akamshika mtoto mkono, akamwambia, “Talitha koum!” (maana yake, “Msichana, nakuambia: amka!”) 42Mara yule msichana akasimama, akaanza kutembea (alikuwa na umri wa miaka kumi na mbili). Walipoona haya, wakastaajabu sana. 43Isa akawaagiza kwa ukali wasimweleze mtu yeyote jambo hilo, naye akawaambia wampe yule msichana chakula.

Iliyochaguliwa sasa

Marko 5: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia