Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 8

8
Isa alisha wanaume 4,000
(Mathayo 15:32-39)
1Katika siku hizo, umati mkubwa wa watu walikusanyika tena. Kwa kuwa walikuwa hawana chakula, Isa akawaita wanafunzi wake akawaambia, 2“Ninahurumia umati huu wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa nami kwa muda wa siku tatu na hawana chakula. 3Nikiwaaga waende nyumbani bila kula, watazimia njiani kwa sababu baadhi yao wametoka mbali.”
4Wanafunzi wake wakamjibu, “Lakini hapa nyikani tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha?”
5Isa akawauliza, “Mna mikate mingapi?”
Wakajibu, “Tuna mikate saba.”
6Akawaambia watu waketi chini. Akaichukua ile mikate saba na kushukuru, baadaye akaimega na kuwapa wanafunzi wake ili wawagawie watu. Wanafunzi wake wakafanya hivyo. 7Walikuwa pia na visamaki vichache, Isa akavibariki, akawaamuru wanafunzi wake wawagawie watu. 8Wale watu walikula na kutosheka. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba. 9Watu waliokula walikuwa wapata elfu nne. Baada ya kuwaaga, 10aliingia kwenye mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda sehemu za Dalmanutha.
Mafarisayo waomba ishara
(Mathayo 12:38-42)
11Mafarisayo#8:11 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. wakaja, wakaanza kumhoji Isa. Ili kumtega, wakamwomba awaoneshe ishara kutoka mbinguni. 12Akahuzunika moyoni, akawaambia, “Kwa nini kizazi hiki kinataka ishara? Amin nawaambieni, hakitapewa ishara yoyote.” 13Kisha akawaacha, akarudi kwenye mashua, akavuka hadi ng’ambo.
Chachu ya Mafarisayo na ya Herode
(Mathayo 16:5-12)
14Wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate ya kutosha. Walikuwa na mkate mmoja tu kwenye mashua. 15Isa akawaonya: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na ya Herode.”
16Wakajadiliana wao kwa wao, na kusema, “Anasema hivi kwa sababu hatukuleta mikate.”
17Isa, akifahamu majadiliano yao, akawauliza: “Mbona mnajadiliana kuhusu kutokuwa na mikate? Je, bado hamtambui wala hamwelewi? Je, mbona mioyo yenu ni migumu kiasi hicho? 18Je, mna macho lakini mnashindwa kuona, na mna masikio lakini mnashindwa kusikia? Je, hamkumbuki? 19Nilipoimega ile mikate mitano kwa watu elfu tano, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa mabaki?”
Wakamjibu, “Kumi na viwili.”
20“Je, nilipoimega ile mikate saba kwa watu elfu nne, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa mabaki?”
Wakamjibu, “Saba.”
21Ndipo akawauliza, “Je, bado hamwelewi?”
Isa amponya Kipofu huko Bethsaida
22Wakafika Bethsaida na baadhi ya watu wakamleta mtu mmoja kipofu wakamsihi Isa amguse. 23Isa akamshika mkono huyo kipofu akampeleka nje ya kijiji. Baada ya kuyatemea mate macho ya yule kipofu na kumwekea mikono, Isa akamuuliza, “Unaona chochote?”
24Yule kipofu akaangalia, akasema, “Ninaona watu, wanaonekana kama miti inayotembea.”
25Isa akamwekea tena mikono machoni. Kisha macho yake yakafunguka, kuona kwake kukarejea naye akaona kila kitu dhahiri. 26Isa akamtuma nyumbani mwake, akamwambia, “Hata kijijini usiingie.”
Petro amkiri Isa kuwa Al-Masihi
(Mathayo 16:13-20; Luka 9:18-21)
27Isa na wanafunzi wake wakaelekea vijiji vya Kaisaria-Filipi. Walipokuwa njiani, Isa akawauliza, “Watu husema mimi ni nani?”
28Wakamjibu, “Baadhi husema wewe ni Yahya, wengine husema ni Ilya, na bado wengine husema wewe ni mmoja wa manabii.”
29Akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?”
Petro akajibu, “Wewe ndiwe Al-Masihi#8:29 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta..”
30Isa akawaonya wasimwambie mtu yeyote habari zake.
Isa atabiri kifo chake
(Mathayo 16:21-28; Luka 9:22-27)
31Ndipo akaanza kuwafundisha wanafunzi wake kuwa Mwana wa Adamu lazima atapata mateso mengi na kukataliwa na wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa Torati, na kwamba itampasa auawe lakini baada ya siku tatu afufuliwe. 32Aliyasema haya waziwazi. Ndipo Petro akamchukua kando na akaanza kumkemea.
33Lakini Isa akageuka na kuwaangalia wanafunzi wake, na akamkemea Petro. Akasema, “Rudi nyuma yangu, Shetani! Moyo wako hauwazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”
34Ndipo akawaita umati ule wa watu pamoja na wanafunzi wake, akasema, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. 35Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili atayaokoa. 36Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? 37Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? 38Mtu yeyote akinionea aibu mimi na maneno yangu katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu#8:38 Mwana wa Adamu ni jina la Isa Al-Masihi kujishirikisha na udhaifu wa mwanadamu. naye atamwonea aibu wakati atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.”

Iliyochaguliwa sasa

Marko 8: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia