Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 12

12
Mafundisho ya kifamilia na ya kijamii
1Yeyote apendaye kuadibishwa hupenda maarifa,
bali yeye achukiaye kuonywa ni mpumbavu.
2Mtu mwema hupata kibali kutoka kwa Mwenyezi Mungu,
bali Mwenyezi Mungu humhukumu mwenye hila.
3Mtu hathibitiki kutokana na uovu,
bali mwenye haki hataondolewa.
4Mke mwenye tabia nzuri ni taji la mumewe,
bali aaibishaye ni kama uozo
katika mifupa ya mumewe.
5Mipango ya mtu mwadilifu ni ya haki,
bali ushauri wa mwovu ni udanganyifu.
6Maneno ya waovu huotea kumwaga damu,
bali maneno ya waadilifu huwaokoa.
7Watu waovu huondolewa na kutoweka,
bali nyumba ya mwenye haki husimama imara.
8Mtu husifiwa kulingana na hekima yake,
bali watu wenye akili zilizopotoka hudharauliwa.
9Heri mtu wa hali ya chini mwenye mtumishi,
kuliko kujifanya mtu wa hali ya juu nawe huna chakula.
10Mtu mwenye haki hujali mahitaji ya mnyama wake,
bali matendo ya huruma ya mwovu ni ukatili.
11Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele,
bali yeye afuataye mambo ya upuzi hana akili.
12Waovu hutamani mateka ya wapotovu,
bali shina la mwenye haki hustawi.
13Mtu mwovu hunaswa kwa mazungumzo yake ya dhambi,
bali mwenye haki huepuka taabu.
14Kutokana na tunda la midomo yao,
watu hujazwa na mambo mema,
na kazi ya mikono yao huwaletea thawabu.
15Njia ya mpumbavu huonekana sawa
machoni pake mwenyewe,
bali mtu mwenye hekima husikiliza ushauri.
16Mpumbavu huonesha kuudhika kwake mara moja,
bali mtu wa busara hupuuza matukano.
17Shahidi wa kweli hutoa ushuhuda wa kuaminika,
bali shahidi wa uongo husema uongo.
18Maneno ya kipumbavu huchoma kama upanga,
bali ulimi wa mwenye hekima huleta uponyaji.
19Midomo isemayo kweli hudumu milele,
bali ulimi wa uongo hudumu kwa muda mfupi tu.
20Upo udanganyifu katika mioyo
ya wale ambao hupanga mabaya,
bali kuna furaha kwa wale wanaoleta amani.
21Hakuna dhara linalompata mwenye haki,
bali waovu wana taabu nyingi.
22Mwenyezi Mungu anachukia sana midomo idanganyayo,
bali hufurahia watu ambao ni wa kweli.
23Mtu mwenye busara hujihifadhia maarifa yeye mwenyewe,
bali moyo wa wapumbavu hububujika upumbavu.
24Mikono yenye bidii itatawala,
bali uvivu huishia katika kazi za utumwa.
25Moyo wa wasiwasi humlemea mtu,
bali neno la fadhili humfurahisha.
26Mtu mwenye haki ni mwangalifu katika urafiki,
bali njia ya waovu huwapotosha.
27Mtu mvivu haoki mawindo yake,
bali mtu mwenye bidii ana mali ya thamani.
28Katika njia ya haki kuna uzima;
katika mapito hayo kuna maisha ya milele.

Iliyochaguliwa sasa

Mithali 12: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia