Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 15

15
1Jawabu la upole hugeuza ghadhabu,
bali neno liumizalo huchochea hasira.
2Ulimi wa mwenye hekima husifu maarifa,
bali kinywa cha mpumbavu hufoka upumbavu.
3Macho ya Mwenyezi Mungu yako kila mahali,
yakiwaangalia waovu na wema.
4Ulimi uletao uponyaji ni mti wa uzima,
bali ulimi udanganyao huponda roho.
5Mpumbavu hubeza maonyo ya baba yake,
bali yeyote akubaliye maonyo huonesha busara.
6Nyumba ya mwenye haki ina hazina kubwa,
bali mapato ya waovu huwaletea taabu.
7Midomo ya mwenye hekima hueneza maarifa,
bali sivyo ilivyo mioyo ya wapumbavu.
8Mwenyezi Mungu huchukia sana dhabihu za waovu,
bali maombi ya wanyofu humfurahisha Mungu.
9Mwenyezi Mungu huchukia sana njia ya waovu,
bali huwapenda wale wafuatao haki.
10Adhabu kali humngoja yeye aachaye njia;
yeye achukiaye maonyo atakufa.
11Mauti#15:11 yaani Kuzimu; kwa Kiebrania ni Sheol na Uharibifu#15:11 kwa Kiebrania ni Abadon viko wazi mbele za Mwenyezi Mungu:
je, si zaidi sana mioyo ya wanadamu!
12Mwenye mzaha huchukia maonyo;
hatataka shauri kwa mwenye hekima.
13Moyo wenye furaha hufanya uso uchangamke,
bali maumivu ya moyoni huponda roho.
14Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa,
bali kinywa cha mpumbavu hujilisha upumbavu.
15Siku zote za wanaoteswa ni za taabu,
bali moyo mchangamfu una karamu ya kudumu.
16Afadhali kuwa na kidogo pamoja na kumcha Mwenyezi Mungu,
kuliko mali nyingi pamoja na ghasia.
17Afadhali chakula cha mboga mahali palipo na upendo,
kuliko nyama ya ndama aliyenona pamoja na chuki.
18Mtu mwepesi wa hasira huchochea ugomvi,
bali mtu mvumilivu hutuliza ugomvi.
19Njia ya mvivu imezibwa na miiba,
bali njia ya mwenye haki ni barabara kuu.
20Mwana mwenye hekima huleta furaha kwa baba yake,
bali mtu mpumbavu humdharau mama yake.
21Upumbavu humfurahisha mtu ambaye hana akili,
bali mtu mwenye ufahamu hushika njia iliyonyooka.
22Mipango hushindwa kufanikiwa kwa ajili ya kukosa ushauri,
bali kukiwa na washauri wengi hufanikiwa.
23Mtu hupata furaha katika kutoa jibu linalofaa:
je, ni zuri namna gani neno lililotoka kwa wakati wake!
24Mapito ya uzima huelekea juu kwa ajili ya wenye hekima
kumwepusha asiende chini kaburini.
25Mwenyezi Mungu hubomoa nyumba ya mtu mwenye kiburi,
bali huilinda mipaka ya mjane isiguswe.
26Mwenyezi Mungu huchukia sana mawazo ya mwovu,
bali mawazo ya wale walio safi humfurahisha yeye.
27Mtu mwenye tamaa huletea jamaa yake taabu,
bali yeye achukiaye rushwa ataishi.
28Moyo wa mwenye haki hupima majibu yake,
bali kinywa cha mwovu hufoka ubaya.
29Mwenyezi Mungu yuko mbali na waovu,
bali husikia maombi ya wenye haki.
30Mtazamo wa tabasamu huleta furaha moyoni,
nazo habari njema huipa mifupa afya.
31Yeye asikilizaye maonyo yatoayo uzima
atakuwa miongoni mwa wenye hekima.
32Yeye anayedharau maonyo hujidharau mwenyewe,
bali yeyote anayekubali maonyo hupata ufahamu.
33Kumcha Mwenyezi Mungu humfundisha mtu hekima,
nao unyenyekevu huja kabla ya heshima.

Iliyochaguliwa sasa

Mithali 15: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia