Mithali 30:7-17
Mithali 30:7-17 NENO
“Ninakuomba vitu viwili, Ee Mwenyezi Mungu; usininyime kabla sijafa: Uutenge mbali nami udanganyifu na uongo; usinipe umaskini wala utajiri, bali unipe chakula cha kunitosha kila siku. Nisije nikawa na vingi vya kuzidi nikakukana na kusema, ‘Mwenyezi Mungu ni nani?’ Au nisije nikawa maskini nikaiba, nami nikaliaibisha jina la Mungu wangu. “Usimchongee mtumishi kwa bwana wake, asije akakulaani, ukapatilizwa kwalo. “Kuna wanaowalaani baba zao, wala hawawabariki mama zao; ambao ni safi machoni pao wenyewe lakini hawakuoshwa uchafu wao; ambao daima macho yao ni ya kiburi, na kutazama kwao ni kwa dharau; ambao meno yao ni panga na mataya yao yamewekwa visu ili kuwaangamiza maskini katika nchi, na wahitaji kutoka miongoni mwa wanadamu. “Mruba anao binti wawili. Wao hulia daima: ‘Nipe! Nipe!’ “Kuna vitu vitatu visivyotosheka kamwe, naam, viko vinne visivyosema, ‘Yatosha!’: Ni kaburi, tumbo lisilozaa, nchi isiyoshiba maji kamwe, na moto, usiosema kamwe, ‘Yatosha!’ “Jicho lile limdhihakilo baba, lile linalodharau kumtii mama, litang’olewa na kunguru wa bondeni, litaliwa na tai.