Zaburi 29:1-11
Zaburi 29:1-11 NENO
Mpeni Mwenyezi Mungu, enyi mashujaa, mpeni Mwenyezi Mungu utukufu na nguvu. Mpeni Mwenyezi Mungu utukufu unaostahili jina lake; mwabuduni Mwenyezi Mungu katika uzuri wa utakatifu wake. Sauti ya Mwenyezi Mungu iko juu ya maji; Mungu wa utukufu hupiga radi, Mwenyezi Mungu hupiga radi juu ya maji makuu. Sauti ya Mwenyezi Mungu ina nguvu; sauti ya Mwenyezi Mungu ni tukufu. Sauti ya Mwenyezi Mungu huvunja mierezi; Mwenyezi Mungu huvunja vipande vipande mierezi ya Lebanoni. Hufanya Lebanoni irukaruke kama ndama, Sirioni urukaruke kama mwana nyati. Sauti ya Mwenyezi Mungu hupiga kwa miali ya radi. Sauti ya Mwenyezi Mungu hutikisa jangwa; Mwenyezi Mungu hutikisa Jangwa la Kadeshi. Sauti ya Mwenyezi Mungu huzalisha ayala, na huuacha msitu wazi. Hekaluni mwake wote wasema, “Utukufu!” Mwenyezi Mungu huketi akiwa ametawazwa juu ya gharika; Mwenyezi Mungu ametawazwa kuwa Mfalme milele. Mwenyezi Mungu huwapa watu wake nguvu; Mwenyezi Mungu huwabariki watu wake kwa kuwapa amani.