Zaburi 9:1-10
Zaburi 9:1-10 NEN
Ee BWANA, nitakutukuza kwa moyo wangu wote, nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu. Nitafurahi na kushangilia ndani yako. Nitaliimbia sifa jina lako, Ewe Uliye Juu Sana. Adui zangu wamerudi nyuma, wamejikwaa na kuangamia mbele zako. Kwa maana umetetea haki yangu na msimamo wangu; umeketi kwenye kiti chako cha enzi, ukihukumu kwa haki. Umekemea mataifa na kuwaangamiza waovu; umeyafuta majina yao milele na milele. Uharibifu usiokoma umempata adui, umeingʼoa miji yao; hata kumbukumbu lao limetoweka. BWANA anatawala milele, ameweka kiti chake cha enzi apate kuhukumu. Mungu atahukumu ulimwengu kwa haki, atatawala mataifa kwa haki. BWANA ni kimbilio la watu wanaoonewa, ni ngome imara wakati wa shida. Wote wanaolijua jina lako watakutumaini wewe, kwa maana wewe BWANA, hujawaacha kamwe wakutafutao.