Utangulizi
Jina la kitabu hiki kwa Kiebrania ni “Sepher Tehillim,” maana yake “Nyimbo za Sifa.” Jina la Kiyunani ni “Psalmoi,” yaani “Nyimbo zinazoandamana na ala za uimbaji za nyuzi,” na ndiyo kiini cha kitabu hiki. Kila sura ya 150 za kitabu hiki ni ya kipekee tena imekamilika, isipokuwa chache tu.
Zaburi zinaleta hisia mbalimbali kama vile misisimko, hali na mivuto mikubwa tofauti. Kwa kuwa Zaburi zinatokana na uzoefu wa kibinafsi kutoka asili pana hivyo, bado zimekuwa na mvuto mkubwa ulimwenguni wote kwa miaka mingi hivi tangu ziandikwe.
Mara kwa mara Zaburi zimeainishwa kwa kufuata namna fulani za maelezeo au mafundisho. Baadhi ya mapendekezo ya aina zenyewe, na mifano yake ambayo inaweza kuwa msaada mkubwa katika kujifunza zaidi ni kama ifuatavyo:
Kawaida ya ibada na sala 120–130
Kuhusu Masiya 2; 16; 22; 25; 69; 110
Kuomba toba 6; 32; 51
Kumkaribia Mungu binafsi 23; 27; 37
Historia 78; 105–106
Kumsifu Mungu 95; 100; 146–150
Maombi ya mwenye haki 17; 20; 40; 55
Kuna uwezekano mkubwa kwamba makusanyo ya awali yalifanywa na Daudi. Nyongeza nyingine na mpangilio inawezekana vilifanywa na Solomoni, Yehoshafati, Hezekia, Yosia na wengine.
Mwandishi
Daudi: 73, Asafu: 12, Wana wa Kora: 10, Mose: 1, Hemani: 1, Ethani: 1, Solomoni: 2, Hazijulikani: 50.
Kusudi
Kuelezea umuhimu wa mashairi katika sifa, kuabudu na kukiri dhambi mbele za Mungu.
Mahali
Palestina na Babeli.
Tarehe
Kati ya wakati wa Mose (1440 K.K.) na wakati wa utumwa wa Babeli (586 K.K.).
Wahusika Wakuu
Daudi, Asafu, Wana wa Kora, Mose, Hemani na Solomoni.
Wazo Kuu
Kusifu ni kutambua na kutangaza ukuu wa Mungu, kufurahia na kudhihirisha wema wake.
Mambo Muhimu
Zaburi zimeelezea ufunuo wa Mungu, uumbaji, hali ya mwanadamu, wokovu, dhambi na uovu, toba, haki na uadilifu, kuabudu na kusifu, maombi na hukumu.
Mgawanyo
Kitabu I: 1–41
Kitabu II: 42–72
Kitabu III: 73–89
Kitabu IV: 90–106
Kitabu V: 107–150.