Ufunuo 14:6-13
Ufunuo 14:6-13 NENO
Kisha nikamwona malaika mwingine akiruka juu angani, naye alikuwa na Injili ya milele ya kuwatangazia wale wanaoishi duniani: kwa kila taifa, kabila, lugha na jamaa. Akasema kwa sauti kubwa, “Mcheni Mungu na kumpa utukufu, kwa maana saa ya hukumu yake imewadia. Mwabuduni yeye aliyeziumba mbingu, dunia, bahari na chemchemi za maji.” Malaika wa pili akafuata akisema, “Umeanguka! Umeanguka Babeli Mkuu, mji ule ulioyafanya mataifa yote kulewa kwa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake.” Malaika wa tatu akawafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, “Kama mtu yeyote anamwabudu huyo mnyama na sanamu yake na kutiwa chapa yake kwenye paji la uso wake au kwenye mkono wake, yeye pia atakunywa mvinyo wa hasira kali ya Mungu ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake pasipo kuchanganywa na maji. Naye atateswa kwa moto uwakao na kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele za Mwana-Kondoo. Nao moshi wa mateso yao hupanda juu milele na milele. Hakuna mapumziko, mchana wala usiku, kwa wale wamwabuduo huyo mnyama na sanamu yake, au kwa yeyote anayepokea chapa ya jina lake.” Hapa ndipo penye wito wa subira na uvumilivu wa watakatifu; wale wanaozishika amri za Mungu na kudumu katika uaminifu kwa Isa. Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Andika: Wamebarikiwa wafu wafao katika Isa Bwana tangu sasa.” “Naam,” asema Roho wa Mungu, “watapumzika kutoka taabu zao, kwa kuwa matendo yao yatawafuata.”