17
Kahaba mkuu na mnyama
1Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba akaja akaniambia, “Njoo, nitakuonesha adhabu ya yule kahaba mkuu, aliyeketi juu ya maji mengi. 2Yule ambaye wafalme wa dunia walizini naye na watu walioishi duniani walilewa kwa mvinyo wa uzinzi wake.”
3Kisha yule malaika akanichukua katika Roho wa Mungu, akanipeleka jangwani. Huko nikamwona mwanamke mmoja ameketi juu ya mnyama mwekundu aliyejaa majina ya kumkufuru Mungu mwili mzima. Mnyama huyo alikuwa na vichwa saba na pembe kumi. 4Huyo mwanamke alikuwa amevaa mavazi ya rangi ya zambarau na nyekundu, akimetameta kwa dhahabu, vito vya thamani na lulu. Mkononi mwake alikuwa ameshika kikombe cha dhahabu kilichojaa mambo ya machukizo na uchafu wa uzinzi wake. 5Kwenye paji lake la uso palikuwa pameandikwa jina la siri:
Babeli Mkuu,
Mama wa makahaba
na wa machukizo ya dunia.
6Nikaona kuwa huyo mwanamke alikuwa amelewa kwa damu ya watakatifu, yaani damu ya wale watu waliouawa kwa ushuhuda wa Isa.
Nilipomwona huyo mwanamke, nilistaajabu sana. 7Ndipo yule malaika akaniambia, “Kwa nini unastaajabu? Nitakufafanulia siri ya huyo mwanamke na huyo mnyama aliyempanda, mwenye vichwa saba na pembe kumi. 8Huyo mnyama ambaye ulimwona awali alikuwako, lakini sasa hayuko, naye atapanda kutoka lile Shimo na kwenda kwenye maangamizi yake. Watu wanaoishi duniani ambao majina yao hayakuandikwa kwenye kitabu cha uzima tangu kuumbwa kwa ulimwengu watastaajabu kumwona huyo mnyama, kwa maana alikuwako hapo awali, na sasa hayuko, lakini atakuwako baadaye.
9“Hapa ndipo penye wito wa akili pamoja na hekima. Vile vichwa saba ni vilima saba ambavyo huyo mwanamke amevikalia. 10Pia hivyo vichwa saba ni wafalme saba. Watano wamekwisha kuanguka, mmoja yupo, mwingine hajaja bado, lakini atakapokuja atalazimika kukaa kwa muda mfupi. 11Yule mnyama aliyekuwako hapo awali na sasa hayuko, yeye ni mfalme wa nane. Ni miongoni mwa wale saba, naye anaenda kwenye maangamizi yake.
12“Zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme kumi ambao bado hawajapokea ufalme, lakini watapokea mamlaka kuwa wafalme kwa saa moja pamoja na yule mnyama. 13Hawa wana nia moja, nao watamwachia yule mnyama nguvu zao na mamlaka yao. 14Watafanya vita na Mwana-Kondoo, lakini Mwana-Kondoo atawashinda kwa sababu yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme. Yeye atakuwa pamoja na watu wake walioitwa ambao ni wateule wake na wafuasi wake waaminifu.”
15Kisha yule malaika akaniambia, “Yale maji uliyoyaona yule kahaba akiwa ameketi juu yake ni jamaa, makundi ya watu, mataifa na lugha. 16Zile pembe kumi ulizoziona, pamoja na huyo mnyama, watamchukia huyo kahaba, watamfilisi na kumwacha uchi, watamla nyama yake na kumteketeza kwa moto. 17Kwa maana Mungu ameweka mioyoni mwao kutimiza kusudi lake kwa kukubali kumpa yule mnyama mamlaka yao ya utawala hadi maneno ya Mungu yatakapotimia. 18Yule mwanamke uliyemwona ni ule mji mkubwa unaowatawala wafalme wa dunia.”