Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 22

22
Mto wa maji ya uzima
1Kisha yule malaika akanionesha mto wa maji ya uzima, maangavu kama kioo yakitiririka kutoka kwa kile kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo, 2kupitia katikati ya barabara kuu ya huo mji. Kwenye kila upande wa huo mto kulikuwa na mti wa uzima utoao matunda ya aina kumi na mbili, ukizaa matunda yake kila mwezi. Nayo majani ya mti huo ni kwa ajili ya uponyaji wa mataifa. 3Katika mji huo hakutakuwa tena na laana, bali kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo humo na watumishi wake watamtumikia, 4nao watamwona uso wake na Jina lake litakuwa kwenye paji za nyuso zao. 5Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, kwa maana Bwana Mwenyezi Mungu atakuwa nuru yao, nao watatawala milele na milele.
6Kisha yule malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kuaminika na kweli. Mwenyezi Mungu, Mungu wa roho za manabii, alimtuma malaika wake kuwaonesha watumishi wake yale ambayo hayana budi kutukia upesi.”
Bwana Isa anakuja
7“Tazama, naja upesi! Amebarikiwa yeye ayashikaye maneno ya unabii wa kitabu hiki.”
8Mimi, Yohana, ndiye niliyesikia na kuyaona mambo haya. Nilipokwisha kuyasikia na kuyaona, nilianguka chini nikasujudu miguuni pa yule malaika aliyekuwa akinionesha mambo hayo. 9Lakini yeye akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi ni mtumishi pamoja nawe na ndugu zako manabii na wote wanaoyashika maneno ya kitabu hiki. Msujudie Mungu!”
10Kisha akaniambia, “Usiyafunge maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, kwa sababu wakati umekaribia. 11Atendaye mabaya na aendelee kutenda mabaya, aliye mchafu na aendelee kuwa mchafu, yeye atendaye haki na aendelee kutenda haki, na yeye aliye mtakatifu na aendelee kuwa mtakatifu.”
12“Tazama, naja upesi! Thawabu yangu i mkononi mwangu, nami nitampa kila mtu sawasawa na alivyotenda. 13Mimi ni Alfa na Omega, wa Kwanza na wa Mwisho, Mwanzo na Mwisho.
14“Wamebarikiwa wale wafuao mavazi yao, ili wapate haki ya kuuendea huo mti wa uzima na kuuingia huo mji kupitia kwenye malango yake. 15Huko nje wako mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu, na kila mtu apendaye udanganyifu na kuufanya.
16“Mimi, Isa, nimemtuma malaika wangu kushuhudia mambo haya kwa ajili ya jumuiya ya waumini. Mimi ndimi Shina na Mzao wa Daudi, ile Nyota ya Asubuhi inayong’aa.”
17Roho wa Mungu na bibi arusi wanasema, “Njoo!” Naye asikiaye na aseme, “Njoo!” Yeyote mwenye kiu na aje, na kila anayetaka na anywe maji ya uzima bure.
18Namwonya kila mtu asikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki: Mtu yeyote akiongeza humo chochote, Mungu atamwongezea mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. 19Kama mtu yeyote akipunguza humo chochote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima na katika ule Mji Mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.
20Yeye anayeshuhudia mambo haya asema, “Hakika, naja upesi!”
Amen. Njoo, Bwana Isa.
21Neema ya Bwana Isa iwe na watakatifu wote. Amen.

Iliyochaguliwa sasa

Ufunuo 22: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia