Ufunuo 5:1-7
Ufunuo 5:1-7 NENO
Kisha nikaona katika mkono wake wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, kitabu kilichoandikwa ndani na nje, kikiwa kimefungwa kwa mihuri saba. Nami nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kuu, “Ni nani anayestahili kuivunja hiyo mihuri na kukifungua kitabu?” Lakini hapakuwa na yeyote mbinguni wala duniani au chini ya dunia aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala hata kutazama ndani yake. Nikalia sana kwa sababu hakuonekana yeyote anayestahili kukifungua hicho kitabu wala kutazama ndani yake. Kisha, mmoja wa wale wazee akaniambia, “Usilie! Tazama, Simba wa kabila la Yuda, wa Uzao wa Daudi, ameshinda. Yeye ndiye anayeweza kukifungua hicho kitabu na kuvunja mihuri yake saba.” Ndipo nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale viumbe wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, akiwa kama amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba, ambazo ndizo zile Roho saba za Mungu zilizotumwa duniani pote. Huyo Mwana-Kondoo akaja na kukitwaa kile kitabu kutoka mkono wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi.