Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 5:8-14

Ufunuo 5:8-14 NENO

Alipokwisha kukitwaa kile kitabu, wale viumbe wenye uhai wanne pamoja na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele ya yule Mwana-Kondoo. Kila mmoja wao alikuwa na kinubi, nao walikuwa wameshika mabakuli ya dhahabu yaliyojaa uvumba, ambayo ni maombi ya watakatifu. Nao wakaimba wimbo mpya, wakisema: “Wewe unastahili kukitwaa kitabu na kuivunja mihuri yake, kwa sababu ulichinjwa, na kwa damu yako ukamnunulia Mungu watu kutoka kila kabila, kila lugha, kila jamaa na kila taifa. Wewe umewafanya hawa wawe ufalme na makuhani wa kumtumikia Mungu wetu, nao watatawala duniani.” Kisha nikatazama, nikasikia sauti za malaika wengi wakiwa wamekizunguka kile kiti cha enzi, pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne. Idadi yao ilikuwa kumi elfu mara kumi elfu na maelfu ya maelfu. Nao waliimba kwa sauti kuu, wakisema: “Anastahili Mwana-Kondoo, yeye aliyechinjwa, kupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na sifa!” Kisha nikasikia kila kiumbe mbinguni na duniani, chini ya nchi, na baharini, na vyote vilivyomo, vikiimba: “Sifa na heshima na utukufu na uweza ni vyake yeye aliyeketi juu ya hicho kiti cha enzi, na kwa Mwana-Kondoo, milele na milele!” Wale viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amen!” Nao wale wazee wakaanguka kifudifudi wakaabudu.