Warumi 4:1-25
Warumi 4:1-25 NENO
Tuseme nini basi, kuhusu Ibrahimu baba yetu kwa jinsi ya mwili: yeye alipataje kujua jambo hili? Kwa maana ikiwa Ibrahimu alihesabiwa haki kwa matendo, basi, anacho kitu cha kujivunia, lakini si mbele za Mungu. Kwa maana Maandiko yasemaje? “Ibrahimu alimwamini Mungu, na ikahesabiwa kwake kuwa haki.” Basi mtu afanyapo kazi, mshahara wake hauhesabiwi kwake kuwa ni zawadi, bali ni haki yake anayostahili. Lakini kwa mtu ambaye hafanyi kazi na anamtumaini Mungu, yeye ambaye huwahesabia waovu haki, imani yake inahesabiwa kuwa haki. Daudi pia alisema vivyo hivyo aliponena kuhusu baraka za mtu ambaye Mungu humhesabia haki pasipo matendo: “Wamebarikiwa wale ambao wamesamehewa makosa yao, ambao dhambi zao zimefunikwa. Heri mtu yule Mwenyezi Mungu hamhesabii dhambi zake.” Je, huku kubarikiwa ni kwa wale waliotahiriwa peke yao, au pia na kwa wale wasiotahiriwa? Tumesema imani ya Ibrahimu ilihesabiwa kwake kuwa haki. Je, ilihesabiwaje kwake kuwa haki? Ni kabla ya kutahiriwa, au baada yake kutahiriwa? Haikuwa baada yake kutahiriwa, bali kabla hajatahiriwa! Alipewa ishara ya tohara kuwa muhuri wa haki aliyokuwa nayo kwa imani hata alipokuwa bado hajatahiriwa. Kusudi lilikuwa kumfanya baba wa wote waaminio pasipo kutahiriwa, ili wahesabiwe kuwa wenye haki. Vivyo hivyo awe baba wa wale waliotahiriwa ambao si kwamba wametahiriwa tu, bali pia wanafuata mfano wa imani ambayo baba yetu Ibrahimu alikuwa nayo kabla ya kutahiriwa. Kwa maana ile ahadi kwamba angeurithi ulimwengu haikuja kwa Ibrahimu au kwa wazao wake kupitia kwa sheria bali kupitia kwa haki ipatikanayo kwa imani. Kwa maana ikiwa wale wanaoishi kwa sheria ndio warithi, imani haina thamani na ahadi haifai kitu, kwa sababu sheria huleta ghadhabu. Mahali ambapo hakuna sheria, hakuna makosa. Kwa hiyo, ahadi huja kupitia kwa imani, ili iwe ni kwa neema, na ihakikishiwe wazao wote wa Ibrahimu, si kwa wale walio wa sheria peke yao, bali pia kwa wale walio wa imani ya Ibrahimu. Yeye ndiye baba yetu sisi sote. Kama ilivyoandikwa: “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.” Yeye ni baba yetu mbele za Mungu, ambaye yeye alimwamini, yule Mungu anayefufua waliokufa, na kuvitaja vitu ambavyo haviko kana kwamba viko. Akitarajia yasiyoweza kutarajiwa, Ibrahimu akaamini, akawa baba wa mataifa mengi, kama alivyoahidiwa kwamba, “Hivyo ndivyo uzao wako utakavyokuwa.” Ibrahimu hakuwa dhaifu katika imani hata alipofikiri hali ya mwili wake, ambao ulikuwa kama uliokufa, kwani umri wake ulikuwa unakaribia miaka mia moja, au alipofikiri hali ya kufa ya tumbo la Sara. Lakini Ibrahimu hakusitasita kwa kutokuamini ahadi ya Mungu, bali alitiwa nguvu katika imani yake na kumpa Mungu utukufu, akiwa na hakika kabisa kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kutimiza lile aliloahidi. Hii ndio sababu, “ilihesabiwa kwake kuwa haki.” Maneno haya “ilihesabiwa kwake kuwa haki,” hayakuandikwa kwa ajili yake peke yake, bali kwa ajili yetu sisi pia ambao Mungu atatupatia haki, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Isa Bwana wetu kutoka kwa wafu. Alitolewa afe kwa ajili ya dhambi zetu, naye alifufuliwa kutoka mauti ili tuhesabiwe haki.