Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mdo 21

21
Safari ya Paulo kwenda Yerusalemu
1Ikawa tulipokwisha kujitenga nao na kuabiri, tukafika Kosi kwa tanga moja, na siku ya pili yake tukafika Rodo na kutoka huko tukafika Patara, 2tukapata merikebu itakayovuka mpaka Foinike tukapanda tukatweka. 3Na tulipoona Kipro tukaiacha upande wa kushoto; tukasafiri mpaka Shamu tukashuka Tiro. Kwa maana huko ndiko merikebu yetu itakakoshusha shehena yake. 4#Mdo 11:12; 20:23Tukiisha kuwaona wanafunzi tukakaa huko siku saba, nao wakamwambia Paulo kwa uweza wa Roho asipande kwenda Yerusalemu. 5#Mdo 20:36Hata tulipotimiza siku zile tukaondoka tukaenda zetu, na watu wote, pamoja na wake zao na watoto wao, wakatusindikiza mpake nje ya mji, tukapiga magoti pwani tukaomba; 6na baada ya kuagana tukapanda merikebuni, nao wakarudi kwao.
7Hata tulipomaliza safari yetu kutoka Tiro tukafika Tolemai, tukawaamkua ndugu tukakaa kwao siku moja. 8#Mdo 6:5; 8:5,40Asubuhi yake tukaondoka, tukafika Kaisaria, tukaingia nyumbani mwa Filipo, mhubiri wa Injili, aliyekuwa mmoja wa wale saba, tukakaa kwake.
9 # Mdo 2:17 Mtu huyu alikuwa na binti wanne, mabikira, waliokuwa wakitabiri. 10#Mdo 11:28Basi tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi. 11#Mdo 20:23Alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa. 12#Mt 16:22Basi tuliposikia haya, sisi na watu wa mahali pale, tukamsihi asipande kwenda Yerusalemu. 13#Mdo 20:24Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu. 14#Mt 26:39; Yn 21:18Alipokataa shauri letu, tukanyamaza tukisema, Mapenzi ya Bwana na yatendeke.
15Baada ya siku zile tukachukua vyombo vyetu tukapanda kwenda Yerusalemu. 16Baadhi ya wanafunzi wa Kaisaria wakafuatana na sisi, wakamchukua na Mnasoni, mtu wa Kipro, mwanafunzi wa zamani ambaye ndiye tutakayekaa kwake.
Paulo Amtembelea Yakobo Yerusalemu
17Tulipofika Yerusalemu wale ndugu wakatukaribisha kwa furaha. 18#Mdo 15:13; Gal 1:19Hata siku ya pili yake Paulo akaingia kwa Yakobo pamoja nasi, na wazee wote walikuwako. 19Na baada ya kuwaamkua, akawaeleza mambo yote moja moja Mungu aliyoyatenda katika Mataifa kwa huduma yake. 20#Mdo 15:1Nao waliposikia wakamtukuza Mungu, wakamwambia, Ndugu yetu, unaona jinsi Wayahudi walioamini walivyo elfu nyingi, nao wote wana wivu sana kwa ajili ya torati. 21#Mdo 16:3; Rum 10:4Nao wameambiwa habari zako, ya kwamba unawafundisha Wayahudi wote wakaao katika Mataifa kumwacha Musa, ukiwaambia wasiwatahiri watoto wao, wala wasizifuate desturi. 22Basi, ni nini? Bila shaka watasikia kwamba umekuja. 23#Hes 6:13-21Basi fanya neno hili tunalokuambia. Wako kwetu watu wanne waliofungwa na nadhiri. 24#Mdo 18:18Wachukue watu hao, ujitakase pamoja nao, na kuwagharimia ili wanyoe vichwa vyao, watu wote wapate kujua ya kuwa habari zile walizoambiwa juu yako si kitu, bali wewe mwenyewe unaenenda vizuri na kuishika torati. 25#Mdo 15:20,29Lakini kwa habari za watu wa Mataifa walioamini, tuliandika na kutoa hukumu yetu ya wao kujilinda nafsi zao na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na kitu kilichosongolewa, na uasherati. 26#Hes 6:1-20; 1 Kor 9:20Ndipo Paulo akawatwaa wanaume wale, na siku ya pili yake akajitakasa nafsi yake pamoja nao, akaingia ndani ya hekalu, akitangaza habari ya kutimiza siku za utakaso, hata sadaka itolewe kwa ajili ya kila mmoja wao.
Paulo Ashikwa akiwa Hekaluni
27Basi zile siku saba zilipokuwa karibu kutimia, Wayahudi waliotoka Asia wakamwona ndani ya hekalu, wakawataharakisha watu wote, wakamkamata, 28#Mdo 6:13; Eze 44:7wakapiga kelele, na kusema, Enyi wanaume wa Israeli, tusaidieni. Huyu ndiye mtu yule afundishaye watu wote kila mahali kinyume cha taifa letu na torati na mahali hapa. Tena, zaidi ya haya, amewaingiza Wayunani katika hekalu, akapatia unajisi mahali hapa patakatifu. 29#Mdo 20:4; 2 Tim 4:20Kwa maana walikuwa wamemwona Trofimo, Mwefeso, pamoja naye mjini, ambaye walidhania ya kuwa Paulo amemwingiza katika hekalu. 30Mji wote ukataharuki, watu wakakutanika mbio mbio, wakamkamata Paulo, wakamkokota, wakamtoa hekaluni; mara milango ikafungwa. 31Na walipokuwa wakitafuta njia ya kumwua, habari zikamfikilia jemadari wa kikosi ya kwamba Yerusalemu imechafuka, mji mzima. 32Mara akatwaa askari na maakida, akawashukia mbio. Nao walipomwona jemadari na askari wakaacha kumpiga Paulo. 33#Mdo 21:11; 20:23Kisha jemadari akakaribia, akamshika, akaamuru afungwe kwa minyororo miwili; akauliza, Nani huyu? Tena, amefanya nini? 34Wengine katika makutano wakapiga kelele wakisema hivi, na wengine hivi. Basi alipokuwa hawezi kupata hakika ya habari kwa sababu ya zile kelele, akatoa amri aletwe ndani ya ngome. 35Basi Paulo alipofika darajani ilikuwa kuchukuliwa na askari kwa sababu ya nguvu ya makutano. 36#Mdo 22:22; Lk 23:18Maana kundi kubwa la watu wakamfuata, wakipiga kelele, na kusema, Mwondoe huyu.
Paulo Ajitetea
37Naye alipokuwa analetwa ndani ya ngome, Paulo akamwambia jemadari, Nina ruhusa nikuambie neno? Naye akasema, Je! Unajua Kiyunani? 38#Mdo 5:36,37Wewe si yule Mmisri ambaye kabla ya siku hizi aliwafitinisha wale watu elfu nne, walioitwa Wauaji, akawaongoza jangwani? 39#Mdo 9:11Paulo akasema, Mimi ni mtu wa Kiyahudi, mtu wa Tarso, mji wa Kilikia, mwenyeji wa mji usiokuwa mnyonge. Nakuomba, nipe ruhusa niseme na wenyeji hawa. 40Basi, alipompa ruhusa, Paulo akasimama madarajani, akawapungia mkono wale wenyeji; na ilipokuwa kimya kabisa, akanena nao kwa lugha ya Kiebrania, akisema,

Iliyochaguliwa sasa

Mdo 21: SUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia