Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Eze 1:1-14

Eze 1:1-14 SUV

Ikawa katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, nilipokuwa pamoja na watu waliohamishwa, karibu na mto Kebari, mbingu zilifunuka, nikaona maono ya Mungu. Siku ya tano ya mwezi, nao ulikuwa ni mwaka wa tano wa kuhamishwa kwake mfalme Yehoyakini, neno la BWANA lilimjia Ezekieli, kuhani, mwana wa Buzi, kwa dhahiri, katika nchi ya Wakaldayo, karibu na mto Kebari; na mkono wa BWANA ulikuwa hapo juu yake. Nikaona, na tazama, upepo wa dhoruba ulitoka upande wa kaskazini, wingu kubwa sana, pamoja na moto, ukifanya duara ya nuru, na mwangaza pande zote, na katikati yake kitu kama rangi ya kaharabu, katikati ya moto huo. Kukatokea katikati yake mfano wa viumbe hai vinne. Kuonekana kwao kulikuwa hivi; walikuwa na sura ya mwanadamu. Na kila mmoja alikuwa na nyuso nne, na kila mmoja alikuwa na mabawa manne. Na miguu yao ilikuwa miguu iliyonyoka; na nyayo za miguu yao zilikuwa kama nyayo za miguu ya ndama; zikimetameta kama rangi ya shaba iliyosuguliwa sana. Nao walikuwa na mikono ya mwanadamu chini ya mabawa yao, pande zote nne; na wote wanne walikuwa na nyuso zao na mabawa yao hivi; mabawa yao yaliungana, hili na hili; nao hawakugeuka walipokwenda, walikwenda kila mmoja kuelekea mbele. Kwa habari za mfano wa nyuso zao; walikuwa na uso wa mwanadamu; na hao wanne walikuwa na uso wa simba upande wa kuume; na hao wanne walikuwa na uso wa ng’ombe upande wa kushoto; na hao wanne walikuwa na uso wa tai pia. Na nyuso zao na mabawa yao yalikuwa yametengana kwa juu; mabawa mawili ya kila mmoja yaliungana, hili na hili, na mawili yalifunika miili yao. Nao walikwenda kuelekea mbele, kila mmoja wao; roho ilikotaka kwenda ndiko walikokwenda; hawakugeuka walipokwenda. Kwa habari za kuonekana kwao vile viumbe hai; kuonekana kwao kulikuwa kama makaa ya moto yawakayo, kama kuonekana kwa vinga vya moto; moto ule ulikuwa ukienda juu na kushuka chini, katikati ya vile viumbe hai; na ule moto ulikuwa na mwangaza mwingi, na katika ule moto ulitoka umeme. Na vile viumbe hai walipiga mbio, kwenda na kurudi, kama kuonekana kwa kumulika kwa umeme.

Soma Eze 1

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Eze 1:1-14