UTANGULIZI
Jina Hosea maana yake ni “wokovu”. Hosea ni mzawa wa Ufalme wa Kaskazini uitwao Israeli. Alihubiri huko Israeli mnamo sehemu ya pili ya karne ya nane Kabla ya Kristo Kuzaliwa.
Wafalme Yeroboamu II wa Israeli na Uzia wa Yuda (pengine anaitwa Azaria) walitawala karibu wakati mmoja mwanzoni mwa karne ya nane Kabla ya Kristo Kuzaliwa. Wote walitawala kwa muda mrefu na utawala wao ulikuwa na mafanikio kwa jinsi yake. Nchi zao zilikuwa imara kisiasa, walipanua mipaka ya nchi zao na biashara ilistawi (tazama 2 Fal 14:23-29; 15:1-2; 2 Nya 26:1-15). Hata hivyo uchaji, dini na uadilifu vilikosekana. Haki na kweli hazikuwapo kabisa. Choyo, tamaa ya mali, magendo na rushwa vilishamiri. Watu wasiokuwa na uwezo kiuchumi hawakutendewa haki ila walinyanyaswa, walionewa na kukandamizwa (4:1-2). Viongozi wa dini hawakuwa waadilifu (6:8-9). Ibada kwa miungu zilienea sehemu nyingi na waisraeli waliweka kando Agano (7:14-16; 8:5-6; 13:6).
Ujumbe wa Hosea unashutumu uasi, uvunjaji wa Agano, kutokuwa na imani kwa Mungu na ukosefu wa uadilifu. Hali hii, Hosea anaieleza kwa mfano wa maisha ya ndoa iliyovunjika. Kama Gomeri alivyomgeuka mumewe, akakosa uaminifu, akavunja agano la ndoa, akawa kahaba. Vile vile furaha ya uasi wa Gomeri ilivyokuwa ya kitambo tu, maana baadaye aliuzwa akawa mjakazi. Pamoja na hali hiyo mume akawa mwaminifu aliendelea kumpenda mkewe aliyeasi, mwishoni alimkomboa Gomeri kutoka utumwani akawa mkewe tena (13:1-3). Ndivyo Waisraeli walivyomwasi na kumwacha Mungu wakavunja Agano wakawa na zinaa ya kiroho (1:2; 2:2). Mungu kwa upendo wake mkuu atawakomboa, atawatakasa unajisi wao wa zinaa na miungu, watarudishwa na kuishi katika nchi yao na kuwa na uhusiano mpya na Mungu wao (2:17-20; 3:4-5; 14:4-7).
Yaliyomo:
1. Ndoa ya Hosea na mafundisho yake, Sura 1-3
2. Dhambi ya Israeli, Sura 4-8
3. Hukumu dhidi ya uasi, Sura 9-13
4. Upendo wa Mungu husamehe, Sura 14