Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isa 53

53
1 # 1 Kor 1:18; Yn 12:38; Rum 10:16 Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta?
Na mkono wa BWANA amefunuliwa nani?
2 # Mk 9:12 Maana alikua mbele zake kama mche mwororo,
Na kama mzizi katika nchi kavu;
Yeye hana umbo wala uzuri;
Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani.
3 # Zab 22:6; Ebr 4:15; Yn 1:10 Alidharauliwa na kukataliwa na watu;
Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko;
Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao,
Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.
4 # Mt 8:17; 26:66; 1 Pet 2:24 Hakika ameyachukua masikitiko yetu,
Amejitwika huzuni zetu;
Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa,
Amepigwa na Mungu, na kuteswa.
5 # 1 Pet 2:24 Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu,
Alichubuliwa kwa maovu yetu;
Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake,
Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.
6 # 1 Pet 2:25 Sisi sote kama kondoo tumepotea;
Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe;
Na BWANA ameweka juu yake
Maovu yetu sisi sote.
7 # Mdo 8:32; 1 Pet 1:19; Ufu 5:6 Alionewa, lakini alinyenyekea,
Wala hakufunua kinywa chake;
Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni,
Na kama vile kondoo anyamazavyo
Mbele yao wakatao manyoya yake;
Naam, hakufunua kinywa chake.
8 # Dan 9:26 Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa;
Na maisha yake ni nani atakayeisimulia?
Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai;
Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu.
9 # Mt 27:57; 1 Pet 2:22 Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya;
Na pamoja na matajiri katika kufa kwake;
Ingawa hakutenda jeuri,
Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.
10 # 2 Kor 5:21; Gal 3:13; Rum 6:9; Efe 1:5 Lakini BWANA aliridhika kumchubua;
Amemhuzunisha;
Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi,
Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi,
Na mapenzi ya BWANA yatafanikiwa mkononi mwake;
11 # Yn 17:3; 1 Yoh 2:1; Rum 5:18 Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika.
Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki
Atawafanya wengi kuwa wenye haki;
Naye atayachukua maovu yao.
12 # Flp 2:9; Kol 2:15; Mk 15:28; Lk 22:37; 23:34 Kwa hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu,
Naye atagawanya nyara pamoja nao walio hodari;
Kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa,
Akahesabiwa pamoja na hao wakosao.
Walakini alichukua dhambi za watu wengi,
Na kuwaombea wakosaji.

Iliyochaguliwa sasa

Isa 53: SUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia