UTANGULIZI
Yeremia, maana yake ni, “Bwana alifanya makubwa”. Yeye alikuwa mwana wa Hilkia. Pia yamkinika kwamba alikuwa kuhani. Yeremia alikuwa mwenyeji wa mji mdogo uitwao Anathothi uliokuwa kwenye vilima kaskazini mwa yerusalemu (1 Fal 2:26). Alikuwa mseja (16:1-2). Alipokuwa na umri kama miaka 20 aliitwa na Mungu kuwa nabii.
Nabii Yeremia alianza huduma yake huko Yerusalemu wakati wa utawala wa mfalme Yosia (640-608 Kabla ya Kristo). Aliendelea na kazi ya unabii kwa watawala waliofuata kwa muda wa miongo minne. (Kuhusu hali ya wakai huo angalia 2 Fal 22–25 na 2 Nya 34–36). Mfalme Yosia alipofanya matengenezo ya dini, Yeremia alisema kuwa matendo ya dini ni mazuri lakini lililo muhimu zaidi ni badiliko la moyoni mwa atendaye matendo hayo pamoja na uadilifu.
Wakati huo, sehemu ya kaskazini mwa Yuda Wababeli walishinda Waashuri na kusini Wamisri walikuwa taifa kubwa lenye nguvu. Yeremia aliambia yuda kuwa utawala wa Babeli umepata nguvu kijeshi ili kuwa chombo cha hukumu ya Mungu kwa dhambi za Yuda. Ilivyo, Yuda hawana budi kujikabidhi kwa Wababeli (21:1-10). Wapinzani wa Yeremia walimwona kuwa ni msalii wa taifa lao. Wachache sana walimwunga mkono. Lakini walio wengi walimlaani (15:10), walimhesabu kuwa nabii wa uongo. Viongozi wa dini na Serikali hata walio wa jamaa yake walifanya njama za kumwua (36:26; 38:4-6,15; 11:18-20). Alifungwa gerezani. Hata hivyo, Wababeli waliteka Yuda. Yerusalemu iliangamizwa na watu walichukuliwa utumwani Babeli. Yeremia alifia Misri (42:19; 43:2,5-6).
Unabii wa Yeremia haukuandikwa kwa kufuata utaratibu wa jinsi ulivyotolewa ila umechanganywa. Ujumbe wake ni kuwa Mungu ni mtakatifu na mwenye rehema. Hafurahi watu wahukumiwe bali waokolewe wamwabudu yeye na kuwa na adili. Mungu huchukia dhambi na huhukumu wee wasiobadili nia na matendo ya maovu. Yeremia alilia na kuombeleza alipoona maafa yanayoijia Yuda. Vivevile alisema kuwa Yuda itachukuliwa utumwani Babeli. Baada ya miaka sabini Babeli itaangamizwa na Wayahudi watarudi katika nchi yao. Kuna mkazo wa pekee kuhusu Agano Jipya (31:31-34 linganisha na Waebrania 8:8-12).
Yaliyomo
1. Kuitwa kwa Yeremia, Sura 1
2. Mungu atahukumu Yuda na Yerusalemu, Sura 2–20
3. Dhambi za viongozi, Sura 21–25
4. Unabii kuhusu uhamisho na uhuru, Sura 26–33
5. Matukio kabla na baada ya kuanguka kwa Yerusalemu, Sura 34–45
6. Ujumbe dhidi ya mataifa ya kigeni, Sura 46–51
7. Nyongeza za historia, Sura 52