Omb 2
2
Maonyo ya Mungu Yatimizwa
1 #
Mt 11:23; 2 Sam 1:19; 1 Nya 28:2 Jinsi Bwana alivyomfunika binti Sayuni
Kwa wingu katika hasira yake!
Ameutupa toka mbinguni hata nchi
Huo uzuri wa Israeli;
Wala hakukikumbuka kiti cha miguu yake
Katika siku ya hasira yake.
2 #
Zab 89:39
Bwana ameyameza makao yote ya Yakobo,
Wala hakuona huruma;
Ameziangusha ngome za binti Yuda
Katika ghadhabu yake;
Amezibomoa hata nchi
Ameunajisi ufalme na wakuu wake.
3 #
Ayu 16:15; Zab 74:11 Ameikata pembe yote ya Israeli
Katika hasira yake kali;
Ameurudisha nyuma mkono wake wa kuume
Mbele ya hao adui,
Naye amemteketeza Yakobo kama moto uwakao,
Ulao pande zote.
4 #
Isa 63:10
Ameupinda upinde wake kama adui,
Amesimama na mkono wake wa kuume kama mtesi;
Naye amewaua hao wote
Waliopendeza macho;
Katika hema ya binti Sayuni
Amemimina kani yake kama moto.
5 #
Yer 52:13
Bwana amekuwa mfano wa adui,
Amemmeza Israeli;
Ameyameza majumba yake yote,
Ameziharibu ngome zake;
Tena amemzidishia binti Yuda
Matanga na maombolezo.
6 #
Zab 80:12; Sef 3:18; Isa 5:5; 1:8 Naye ameondoa maskani yake kwa nguvu,
Kana kwamba ni ya bustani tu;
Ameziharibu sikukuu zake;
BWANA amezisahauzisha katika Sayuni
Sikukuu za makini na sabato;
Naye amewadharau mfalme na kuhani
Katika uchungu wa hasira yake.
7 #
Zab 78:59-61; Eze 7:20; Isa 64:10,11; Mik 3:12; Yer 7:12-14; Mt 24:2; Zab 74:4 Bwana ameitupilia mbali madhabahu yake,
Amepachukia patakatifu pake;
Amezitia katika mikono ya hao adui
Kuta za majumba yake;
Wamepiga kelele ndani ya nyumba ya BWANA
Kama katika siku ya kusanyiko la makini.
8 #
Isa 34:11; Amo 7:7 BWANA amekusudia kuuharibu
Ukuta wa binti Sayuni;
Ameinyosha hiyo kamba,
Hakuuzuia mkono wake usiangamize;
Bali amefanya boma na ukuta kuomboleza;
Zote pamoja hudhoofika.
9 #
Kum 28:36; 2 Fal 25:7; 2 Nya 15:3; Zab 74:9; Amo 8:11,12; Mik 3:6,7 Malango yake yamezama katika nchi;
Ameyaharibu makomeo yake na kuyavunja;
Mfalme wake na wakuu wake wanakaa
Kati ya mataifa wasio na sheria;
Naam, manabii wake hawapati maono
Yatokayo kwa BWANA.
10 #
Ayu 2:13; Omb 4:5; Isa 47:1-5 Wazee wa binti Sayuni huketi chini,
Hunyamaza kimya;
Wametupa mavumbi juu ya vichwa vyao,
Wamejivika viunoni nguo za magunia;
Wanawali wa Yerusalemu huinama vichwa vyao
Kuielekea nchi.
11 #
Zab 6:7; Ayu 16:13 Macho yangu yamechoka kwa machozi,
Mtima wangu umetaabika;
Ini langu linamiminwa juu ya nchi
Kwa uharibifu wa binti ya watu wangu;
Kwa sababu watoto wachanga na wanyonyao,
Huzimia katika mitaa ya mji.
12Wao huwauliza mama zao,
Zi wapi nafaka na divai?
Hapo wazimiapo kama waliojeruhiwa
Katika mitaa ya mji,
Hapo walipomiminika nafsi zao
Vifuani mwa mama zao.
13 #
Ayu 5:1; Dan 9:12 Nikushuhudie nini? Nikufananishe na nini,
Ee Binti Yerusalemu?
Nikusawazishe na nini, nipate kukufariji,
Ee bikira binti Sayuni?
Kwa maana uvunjifu wako ni mkuu kama bahari,
Ni nani awezaye kukuponya?
14 #
Isa 58:1
Manabii wako wameona maono kwa ajili yako
Ya ubatili na upumbavu
Wala hawakufunua uovu wako,
Wapate kurudisha kufungwa kwako;
Bali wameona mabashiri ya ubatili kwa ajili yako
Na sababu za kuhamishwa.
15 #
1 Fal 9:8; Zab 48:2 Hao watu wote wapitao
Hukupigia makofi;
Humzomea binti Yerusalemu,
Na kutikisa vichwa vyao;
Je! Mji huu ndio ulioitwa, Ukamilifu wa uzuri,
Furaha ya dunia yote?
16 #
Zab 56:2; 35:21 Juu yako adui zako wote
Wamepanua vinywa vyao;
Huzomea, husaga meno yao,
Husema, Tumemmeza;
Hakika siku hii ndiyo tuliyoitazamia;
Tumeipata, tumeiona.
17 #
Law 26:16; Zab 38:16; Kum 28:15,43,44; Omb 1:5 BWANA ameyatenda aliyoyakusudia; amelitimiza neno lake,
Aliloliamuru siku za kale;
Ameangusha hata chini,
Wala hakuona huruma;
Naye amemfurahisha adui juu yako,
Ameitukuza pembe ya watesi wako.
18 #
Yer 14:17; Omb 1:16 Mioyo yao ilimlilia Bwana;
Ee ukuta wa binti Sayuni!
Machozi na yachuruzike kama mto
Mchana na usiku;
Usijipatie kupumzika;
Mboni ya jicho lako isikome.
19 #
Mk 13:35; Zab 62:8; Isa 51:20; Omb 4:1; Nah 3:10 Inuka, ulalamike usiku,
Mwanzo wa makesha yake;
Mimina moyo wako kama maji usoni pa Bwana;
Umwinulie mikono yako;
Kwa uhai wa watoto wako wachanga wazimiao kwa njaa,
Mwanzo wa kila njia kuu.
20 #
Kut 32:11; Law 26:29; Kum 28:53; Yer 19:9; Omb 4:10,13 Tazama, BWANA, uangalie,
Ni nani uliyemtenda hayo!
Je! Wanawake wale mazao yao,
Watoto waliowabeba?
Je! Kuhani na nabii wauawe
Katika patakatifu pa Bwana?
21 #
2 Nya 36:17
Kijana na mzee hulala chini
Katika njia kuu;
Wasichana wangu na wavulana wangu
Wameanguka kwa upanga;
Umewaua katika siku ya hasira yako;
Umeua, wala hukuona huruma.
22 #
Zab 31:13; Yer 46:5; Hos 9:12 Umeziita kama katika siku ya mkutano wa makini;
Hofu zangu zije pande zote;
Wala hapana hata mmoja aliyepona wala kusalia
Katika siku ya hasira ya BWANA;
Hao niliowabeba na kuwalea
Huyo adui yangu amewakomesha.
Iliyochaguliwa sasa
Omb 2: SUV
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.