13
Tubuni au Mwangamie
1 #
Mdo 5:37
Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao. 2#Yn 9:2Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? 3#Zab 7:12Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. 4Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu? 5Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.
Mfano wa Mtini Usiozaa Matunda
6 #
Lk 3:9; Mt 3:10; 21:19; Mk 11:13 Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate. 7Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu? 8#2 Pet 3:9,15Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; 9nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate.
Yesu Amponya Mwanamke Mlemavu
10Siku ya sabato alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo. 11Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa. 12Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako. 13#Mk 7:32Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu. 14#Kut 20:9-10; Kum 5:13-14Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu, akawaambia mkutano, Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato. 15#Lk 14:5Lakini Bwana akajibu akasema, Enyi wanafiki, kila mmoja wenu, je! Hamfungui ng’ombe wake au punda wake siku ya sabato katika zizi, aende naye kumnywesha? 16#Lk 19:9; Mdo 3:25Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Ibrahimu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii, haikupasa afunguliwe kifungo hiki siku ya sabato? 17Aliposema haya wakatahayari wote walioshindana naye; mkutano wote wakafurahi kwa sababu ya mambo matukufu yaliyotendwa na yeye.
Mfano wa Punje ya Haradali
18 #
Mt 13:31-33; Mk 4:30-32 Kisha alisema, Ufalme wa Mungu umefanana na nini? Nami niufananishe na nini? 19#Dan 4:12,21; Eze 17:23; 31:6Umefanana na punje ya haradali aliyotwaa mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa angani wakakaa katika matawi yake.
Mfano wa Chachu
20Akasema mara ya pili, Niufananishe na nini ufalme wa Mungu? 21Umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachacha wote pia.
Mlango ulio Mwembamba
22Naye alikuwa akipita katika miji na vijiji, akifundisha, katika safari yake kwenda Yerusalemu. 23Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia, 24#Mt 7:13,14; Flp 3:12; 1 Tim 6:12Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze. 25#Mt 25:11,12Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako; 26#Mt 7:22,23ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu. 27#Zab 6:8Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu. 28#Mt 8:11-12#Mt 22:13; 25:30Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje. 29#Mal 1:11; Isa 49:12; 59:19; Zab 107:3; Lk 14:15Nao watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu. 30#Mt 19:30; 20:16; Mk 10:31Na tazama, wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.
Maombolezo juu ya Yerusalemu
31Saa ile ile Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua. 32Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika. 33Pamoja na hayo imenipasa kushika njia yangu leo na kesho na kesho kutwa; kwa kuwa haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu. 34#Mt 23:37-39Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga kwa mawe waliotumwa kwako, mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako kama vile kuku avikusanyavyo vifaranga vyake chini ya mbawa zake, wala hamkutaka. 35#Zab 69:25; 118:26; Yer 12:7; 22:5Angalieni, mmeachiwa nyumba yenu! Nami nawaambia, Hamtaniona tena kamwe, hata mtakaposema, Amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.