Mk 14:1-11
Mk 14:1-11 SUV
Baada ya siku mbili ilikuwa sikukuu ya Pasaka, na mikate isiyochachwa; wakuu wa makuhani na waandishi wakatafuta njia ya kumkamata kwa hila na kumwua. Kwa maana walisema, Isiwe kwa wakati wa sikukuu, isije ikatokea ghasia katika watu. Naye alipokuwapo Bethania, nyumbani mwa Simoni mkoma, ameketi chakulani, alikuja mwanamke mwenye kibweta cha marhamu ya nardo safi ya thamani nyingi; akakivunja kibweta akaimimina kichwani pake. Palikuwa na watu waliochukizwa katika nafsi zao wakisema, Kwani kupoteza marhamu namna hii? Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa dinari mia tatu na kuzidi, wakapewa maskini. Wakamnung’unikia sana yule mwanamke. Yesu akasema, Mwacheni; mbona mnamtaabisha? Amenitendea kazi njema; maana sikuzote mnao maskini pamoja nanyi, na kila mpendapo mwaweza kuwatendea mema; lakini mimi hamnami sikuzote. Ametenda alivyoweza; ametangulia kuupaka mwili wangu marhamu kwa ajili ya maziko. Amin, nawaambia, Kila ihubiriwapo Injili katika ulimwengu wote, na hili alilotenda huyu litatajwa kwa kumbukumbu lake. Yuda Iskariote, yule mmoja katika wale Thenashara, akaenda zake kwa wakuu wa makuhani, apate kumsaliti kwao. Nao waliposikia walifurahi, wakaahidi kumpa fedha. Akatafuta njia ya kumsaliti wakati wa kufaa.