Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 7:23-39

1 Wafalme 7:23-39 SRUV

Tena akatengeneza bahari ya kusubu, mikono kumi toka ukingo hata ukingo, ikaviringana, na mikono mitano ilikuwa kwenda juu kwake; na uzi wa mikono thelathini kuizunguka kabisa. Na chini ya ukingo wake kulikuwa na maboga yaliyoizunguka, kwa mikono kumi, yakiizunguka bahari; kulikuwa na safu mbili za hayo maboga, yakafanywa katika kalibu hapo bahari ilipofanywa. Ikakaa juu ya ng'ombe kumi na wawili, watatu wakitazama kaskazini, na watatu wakitazama magharibi, na watatu wakitazama kusini, na watatu wakitazama mashariki; na bahari iliwekwa juu yao, na pande zao za nyuma zote zilikuwa ndani. Na unene wake ulikuwa nyanda nne; na ukingo wake ukafanywa kama ukingo wa kikombe, kama ua la yungi; huingia bathi elfu mbili. Akavifanya vile vitako kumi vya shaba; mikono minne urefu wa kitako kimoja, na mikono minne upana wake, na mikono mitatu kwenda juu kwake. Na kazi ya vitako ndiyo hii; vilikuwa na papi; na papi zilikuwa katikati ya vipandio; na juu ya papi zilizokuwa katikati ya vipandio kulikuwa na simba, na ng'ombe, na makerubi; na juu ya vipandio kulikuwa na kitako; na chini ya simba na ng'ombe kulikuwa na masongo ya kazi ya kupembeza. Kila kitako kilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vipini vya shaba; na miguu yake minne ilikuwa na mataruma; chini ya birika yalikuwako mataruma ya kusubu, yenye masongo kila moja mbavuni. Na kinywa chake ndani ya taji na juu yake kilikuwa mkono mmoja; na kinywa chake kikaviringana kama kazi ya vitako, mkono mmoja na nusu; tena juu ya kinywa chake kulikuwa na nakshi, na papi zao zilikuwa za mraba, wala hazikuviringana. Na magurudumu manne yalikuwa chini ya papi; na mikono ya magurudumu ndani ya vitako; na kwenda juu kwake gurudumu moja mkono mmoja na nusu. Na kazi ya magurudumu ilikuwa kama kazi ya gurudumu la gari; mikono yake, na maduara, na matindi, na vipande vya ndani, vyote vilikuwa vya kusubu. Kulikuwa na mataruma manne katika pembe nne za kitako kimoja; mataruma hayo ni kitu kimoja na kitako chenyewe. Na juu ya kitako kulikuwa na duara nusu mkono kwenda juu kwake; na juu ya kitako mashikio yake na papi zake vilikuwa vya namna iyo hiyo. Akachora juu ya mabamba ya mashikio yake, na juu ya papi zake, makerubi, na simba, na mitende, moja moja kama ilivyokuwa nafasi, na masongo pande zote. Hivyo akavifanya vile vitako kumi; vyote vilikuwa vya kalibu moja, na cheo kimoja, na namna moja. Akafanya birika kumi za shaba; birika moja huingia bathi arubaini; na kila birika ilikuwa mikono minne; birika moja juu ya kitako kimoja, katika vile vitako kumi. Akaviweka vile vitako, vitano upande wa kulia wa nyumba, na vitano upande wa kushoto wa nyumba; akaiweka ile bahari upande wa kulia wa nyumba upande wa mashariki, kuelekea kusini.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 1 Wafalme 7:23-39