2 Wakorintho 6:1-10
2 Wakorintho 6:1-10 SRUV
Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure. (Kwa maana asema, Kwa wakati uliokubalika nilikusikia, Na katika siku ya wokovu nilikusaidia; tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa.) Tusiwe kwazo la namna yoyote katika jambo lolote, ili utumishi wetu usilaumiwe; bali katika kila neno tujipatie sifa njema, kama watumishi wa Mungu; katika subira nyingi, katika mateso, katika shida, katika matatizo; katika mapigo, katika vifungo, katika fitina, katika taabu, katika kukesha, katika kufunga; katika kuwa safi, katika elimu, katika uvumilivu, katika utu wema, katika Roho Mtakatifu, katika upendo usio unafiki; katika neno la kweli, katika nguvu ya Mungu; kwa silaha za haki za mkono wa kulia na za mkono wa kushoto; kwa utukufu na aibu; kwa kunenwa vibaya na kunenwa vema; kama wadanganyao, bali tu watu wa kweli; kama wasiojulikana, bali wajulikanao sana; kama wanaokufa, kumbe tu hai; kama wanaorudiwa, bali wasiouawa; kama wenye huzuni, bali siku zote tu wenye furaha; kama maskini, bali tukitajirisha wengi; kama wasio na kitu, bali tu wenye vitu vyote.