2 Samweli 19:40-43
2 Samweli 19:40-43 SRUV
Hivyo mfalme akavuka, akafika Gilgali; Kimhamu akavuka pamoja naye; na watu wote wa Yuda wakamvusha mfalme, na nusu ya watu wa Israeli. Tena, angalia, watu wote wa Israeli wakamjia mfalme wakamwambia mfalme, Kwa nini ndugu zetu, watu wa Yuda wamekuiba, na kumvusha Yordani mfalme, na jamaa yake, na watu wote wa Daudi pamoja naye? Ndipo watu wote wa Yuda wakawajibu hao watu wa Israeli, Ni kwa sababu mfalme ni wa jamaa yetu; mbona basi ninyi mmekasirika kwa ajili ya jambo hili? Je! Sisi tumekula kitu cha mfalme? Ama ametupa sisi zawadi yoyote? Hao watu wa Israeli wakawajibu watu wa Yuda, wakasema, Sisi tunazo sehemu kumi katika mfalme, tena tunayo haki yetu katika Daudi zaidi kuliko ninyi; mbona basi ninyi mmetudharau sisi, msitake ushauri wetu kwanza katika kumrudisha tena mfalme wetu? Na maneno ya watu wa Yuda yakawa makali kuliko maneno ya watu wa Israeli.