Matendo 3:1-10
Matendo 3:1-10 SRUV
Basi Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali, saa tisa. Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango wa hekalu uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu. Mtu huyu akiwaona Petro na Yohana wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka. Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema, Tutazame sisi. Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao. Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kulia, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu. Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akirukaruka, na kumsifu Mungu. Watu wote wakamwona akienda, akimsifu Mungu. Wakamtambua, ya kuwa yeye ndiye aliyekuwa akiketi na kuomba sadaka penye mlango wa hekalu uitwao Mzuri; wakawa na mshangao na kustaajabia mambo yale yaliyompata.