Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Amosi 6:1-14

Amosi 6:1-14 SRUV

Ole wao wanaostarehe katika Sayuni, na hao wanaokaa salama katika mlima wa Samaria, watu mashuhuri wa taifa lililo la kwanza, ambao nyumba ya Israeli huwaendea. Piteni hadi Kalne, mkaone; tena tokea huko nendeni hadi Hamathi iliyo kuu; kisha shukeni hadi Gathi ya Wafilisti; je! Ninyi ni bora kuliko falme hizi? Au eneo lao ni kubwa kuliko eneo lenu? Ninyi mnaoiweka mbali siku hiyo mbaya, na kulileta karibu kao la udhalimu; ninyi mnaolala juu ya vitanda vya pembe, na kujinyosha juu ya makochi yenu; ninyi mnaokula wana-kondoo wa kundi, na ndama waliomo zizini; ninyi mnaoimba nyimbo za upuzi pamoja na sauti ya vinanda, na kujifanyia vinanda vya namna nyingi, kama vile Daudi; ninyi mnaokunywa divai katika mabakuli, na kujipaka marhamu iliyo nzuri; lakini hawahuzuniki kwa sababu ya mateso ya Yusufu. Basi kwa ajili ya hayo sasa watakwenda utumwani pamoja na wa kwanza watakaokwenda utumwani, na kelele za shangwe za hao waliojinyosha zitakoma. Bwana MUNGU ameapa kwa nafsi yake, asema BWANA, Mungu wa majeshi; Naizira fahari ya Yakobo, nachukizwa na majumba yake; kwa sababu hiyo nitautoa huo mji, pamoja na wote waliomo ndani yake. Hata itakuwa, wakisalia wanaume kumi katika nyumba moja, watakufa. Na mjomba wa mtu atakapomwinua, yaani, yeye amchomaye moto, ili atoe mifupa yake nyumbani, naye atakapomwambia yeye aliye katika pande za ndani za nyumba, Je! Yuko mtu yeyote pamoja nawe? Naye atakaposema, La, hapana; ndipo atasema, Nyamaza kimya; maana hatuna ruhusa kulitaja jina la BWANA. Kwa maana, angalia, BWANA atoa amri, na jumba kuu litabomolewa vipande vipande, na nyumba ndogo kuwa vigae. Je! Farasi watapiga mbio juu ya mwamba? Je! Mtu atalima kwa plau na ng'ombe baharini? Hata mmegeuza hukumu kuwa sumu, na matunda ya haki kuwa uchungu; ninyi mnaolifurahia jambo lisilo na maana, msemao, Je! Hatukujipatia pembe kwa nguvu zetu wenyewe? Maana, angalia, nitaleta taifa juu yenu, enyi nyumba ya Israeli, asema BWANA, Mungu wa majeshi, nao watawatesa ninyi toka mahali pa kuingilia katika Hamathi hata kijito cha Araba.

Soma Amosi 6