Ezekieli 17:1-21
Ezekieli 17:1-21 SRUV
Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, tega kitendawili, ukawaambie nyumba ya Israeli mithali; useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tai mkubwa, mwenye mabawa makubwa na manyoya marefu katika mabawa, mwenye kujaa manyoya, yaliyo ya rangi mbalimbali, alifika Lebanoni, akakitwaa kilele cha mwerezi; akakikata kitawi kilicho juu katika vitawi vyake, akakichukua mpaka nchi ya biashara, akakiweka katika mji wa wachuuzi. Akatwaa tena mbegu katika mbegu za nchi hiyo, akaipanda katika udongo uzaao sana, akaiweka kando ya maji mengi; aliipandikiza kama mti ukuao karibu na mto. Ikakua, ikawa mzabibu wenye kuenea sana, wa kimo kifupi, ambao matawi yake yalimgeukia, na mizizi yake ilikuwa chini yake; basi ukawa mzabibu, ukatoa matawi, ukachipuza vichipuko. Kulikuwa na tai mwingine mkubwa, mwenye mabawa makubwa na manyoya mengi; na tazama, mzabibu huo ukapinda mizizi yake imwelekee yeye, ukachipuza matawi yake yamwelekee yeye, toka matuta yake ulipopandwa; ili yeye apate kuunywesha. Ulikuwa umepandwa katika udongo mwema, kando ya maji mengi, upate kutoa matawi, na kuzaa matunda, uwe mzabibu mzuri. Basi nena wewe, Bwana MUNGU asema hivi; Je! Huo utafanikiwa? Yeye hataing'oa mizizi yake na kuyakata matunda yake, ili ukauke? Kwamba majani mabichi yake yote yachipukayo yakauke, hata ikiwa hana nguvu nyingi, wala watu wengi wa kuung'oa na mizizi yake? Naam, tazama, ingawa umepandwa, je! Utafanikiwa? Hautakauka kabisa, upepo wa mashariki utakapoupiga? Naam, utakauka katika matuta hapo ulipopandwa. Tena neno la BWANA likanijia, kusema, Waambie sasa nyumba hii iliyoasi, Hamjui maana ya mambo haya? Waambie, Tazama, mfalme wa Babeli alifika Yerusalemu, akamtwaa mfalme wake, na wakuu wake, akawachukua pamoja naye mpaka Babeli; akawatwaa baadhi ya wazao wa kifalme; kisha akafanya agano naye, akamwapisha; akawaondoa watu wa nchi wenye nguvu; ili ufalme huo uwe duni usijiinue, lakini usimame kwa kulishika agano lake. Lakini alimwasi kwa kutuma wajumbe huko Misri, wampe farasi na watu wengi. Je! Atafanikiwa? Afanyaye mambo hayo ataokoka? Atalivunja agano, kisha akaokoka? Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hakika mahali pale akaapo mfalme aliyemweka awe mfalme, ambaye alikidharau kiapo chake, na kulivunja agano lake, ndipo atakapokufa pamoja naye kati ya Babeli. Wala Farao na jeshi lake kubwa, na kusanyiko lake kuu la watu, hawatamfaa kitu vitani, watakapofanya maboma, na kujenga ngome, ili kukatilia mbali watu wengi. Kwa maana amekidharau kiapo kwa kulivunja agano; na tazama, ametia mkono wake, na pamoja na hayo ameyatenda mambo hayo yote; hataokoka. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kama mimi niishivyo, hakika kiapo changu alichokidharau, na agano langu alilolivunja, nitampatiliza kichwani pake. Nami nitatandika wavu wangu juu yake, naye atanaswa katika mtego wangu, nami nitamleta hadi Babeli; nami nitateta naye huko kwa sababu ya kosa lake alilonikosa. Na wakimbizi wake wote wa vikosi vyake vyote wataanguka kwa upanga, na hao watakaosalia watatawanyika kwenye kila upepo; nanyi mtajua ya kuwa mimi, BWANA, nimenena neno hili.