Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 20:18-32

Ezekieli 20:18-32 SRUV

Kisha nikawaambia watoto wao jangwani, Msiende katika amri za baba zenu, wala msizishike hukumu zao, wala msijitie unajisi kwa vinyago vyao. Mimi ni BWANA, Mungu wenu; endeni katika amri zangu, mkazishike hukumu zangu, na kuzitenda; zitakaseni sabato zangu; zitakuwa ishara kati ya mimi na ninyi, mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Lakini watoto hao waliniasi; hawakuenda katika amri zangu, wala hawakuzishika hukumu zangu kuzitenda, ambazo mwanadamu ataishi kwazo kama akizitenda; walizitia unajisi sabato zangu, ndipo nikasema, kwamba nitamwaga ghadhabu yangu juu yao, ili kuitimiza hasira yangu juu yao jangwani. Lakini niliuzuia mkono wangu, nikatenda kwa ajili ya jina langu, lisitiwe unajisi mbele ya macho ya mataifa, ambao mbele ya macho yao niliwatoa. Tena niliwainulia mkono wangu jangwani, kwamba nitawatawanya kati ya mataifa, na kuwatapanya katika nchi mbalimbali; kwa sababu hawakuzitekeleza hukumu zangu, bali walizikataa amri zangu, nao walizitia unajisi sabato zangu, na macho yao yaliandama vinyago vya baba zao. Tena niliwapa amri zisizokuwa njema, na hukumu ambazo hawakuweza kuishi kwazo; nami nikawatia unajisi kwa matoleo yao wenyewe, kwa kuwa walipitisha motoni wote waliofungua tumbo; ili kuwafanya kuwa ukiwa, wakapate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Basi, mwanadamu, sema na nyumba ya Israeli, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Baba zenu wamenitukana kwa jambo hili, kwa kuwa wametenda kosa juu yangu. Kwa maana nilipokuwa nimekwisha kuwaingiza katika nchi ile, ambayo niliuinua mkono wangu kuwapa, wakati huo walipoona kila mlima mrefu, na kila mti wenye majani mengi, walitoa matoleo yao huko, na huko walitoa chukizo la sadaka zao, na huko walifukiza manukato ya kupendeza, na huko walimimina sadaka zao za kunywewa. Ndipo nikawauliza, Nini maana yake mahali palipoinuka mnapopaendea? Basi, jina lake mahali pale ni Bama hata leo. Basi, uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Je! Mnajitia unajisi kwa kuzifuata njia za baba zenu? Mnakwenda kufanya uasherati kwa kuyafuata machukizo yao? Tena mtoapo matoleo yenu, na kuwapitisha watoto wenu motoni, je! Mnajitia unajisi kwa vinyago vyenu vyote hata leo? Na mimi je! Niulizwe neno nanyi, Enyi nyumba ya Israeli? Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sitaulizwa neno na ninyi. Na haya yote yaingiayo katika nia zenu hayatakuwa kamwe; ikiwa mmesema, Sisi tutakuwa sawasawa na mataifa, sawasawa na jamaa za nchi nyingine, kutumikia miti na mawe.