Mwanzo 21:1-13
Mwanzo 21:1-13 SRUV
BWANA akamjia Sara kama alivyonena, na BWANA akamfanyia kama alivyosema. Sara akapata mimba akamzalia Abrahamu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu. Abrahamu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia. Abrahamu akamtahiri Isaka mwanawe, alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwamuru. Naye Abrahamu alikuwa mtu wa miaka mia moja, alipozaliwa mwana wake Isaka. Sara akasema, Mungu amenifanyia kicheko; kila asikiaye atacheka pamoja nami. Akasema, Ni nani angemwambia Abrahamu, Sara atanyonyesha wana? Maana nimemzalia mwana katika uzee wake. Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Abrahamu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya. Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Abrahamu, anafanya dhihaka. Kwa hiyo akamwambia Abrahamu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Abrahamu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Abrahamu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa. Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako.