Mwanzo 48:17-22
Mwanzo 48:17-22 SRUV
Yusufu alipoona kwamba babaye anaweka mkono wake wa kulia juu ya kichwa cha Efraimu, ikawa vibaya machoni pake. Akauinua mkono wa babaye auondoe katika kichwa cha Efraimu, ili auweke juu ya kichwa cha Manase. Yusufu akamwambia babaye, Sivyo, babangu, maana huyu ni mzaliwa wa kwanza; weka mkono wako wa kulia kichwani pake. Babaye akakataa, akasema, Najua, mwanangu najua, yeye naye atakuwa taifa, yeye naye atakuwa mkuu; lakini ndugu yake mdogo atakuwa mkubwa kuliko yeye, na uzao wake watakuwa mataifa mengi Akawabariki siku ile akisema, Katika ninyi Waisraeli watabariki, wakisema, Mungu na akufanye kama Efraimu na kama Manase. Akamweka Efraimu mbele ya Manase. Israeli akamwambia Yusufu, Angalia, mimi ninakufa, lakini Mungu atakuwa pamoja nanyi, naye atawarudisha mpaka nchi ya baba zenu. Nami nimekupa wewe sehemu moja zaidi kuliko ndugu zako, niliyoitwaa katika mikono ya Waamori, kwa upanga wangu na upinde wangu.