Yohana 7:25-36
Yohana 7:25-36 SRUV
Basi baadhi ya watu wa Yerusalemu wakasema, Je! Huyu siye wanayemtafuta ili wamwue? Na kumbe! Anena waziwazi, wala hawamwambii neno! Inawezekana hao wakuu wanajua hakika ya kuwa huyu ndiye Kristo? Lakini huyu twamjua atokako; bali Kristo atakapokuja hakuna ajuaye atokako. Basi Yesu akapaza sauti yake hekaluni, akifundisha na kusema, Mimi mnanijua, na huko nitokako mnakujua; wala sikuja kwa nafsi yangu; ila yeye aliyenituma ni wa kweli, msiyemjua ninyi. Mimi namjua, kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma. Basi wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika, kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado. Na watu wengi katika mkutano wakamwamini; wakasema, Atakapokuja Kristo, je! Atafanya ishara nyingi zaidi kuliko hizi alizozifanya huyu? Mafarisayo wakawasikia mkutano wakinung'unika hivi juu yake; basi wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakatuma watumishi ili wamkamate. Basi Yesu akasema, Bado kitambo kidogo nipo pamoja nanyi; kisha naenda zangu kwake yeye aliyenituma. Mtanitafuta wala hamtaniona; nami nilipo ninyi hamwezi kuja. Basi Wayahudi wakasemezana, Huyu atakwenda wapi hata sisi tusimwone? Ati! Atakwenda kwa Utawanyiko wa Wagiriki, na kuwafundisha Wagiriki? Ni neno gani hilo alilolisema, Mtanitafuta wala hamtaniona; nami nilipo ninyi hamwezi kuja?