Luka 19:28-40
Luka 19:28-40 SRUV
Na alipokwisha kusema hayo, alitangulia mbele akipanda kwenda Yerusalemu. Ikawa alipokaribia Bethfage na Bethania, kwenye mlima uitwao wa Mizeituni, alituma wawili katika wale wanafunzi, akisema, Nendeni mpaka katika kijiji kile kinachowakabili, na mtakapoingia ndani mtaona mwanapunda, amefungwa, ambaye hajapandwa na mtu yeyote bado, mfungueni mkamlete hapa. Na kama mtu akiwauliza, Mbona mnamfungua? Semeni hivi, Bwana anamhitaji. Na wale waliotumwa wakaenda wakaona kama alivyowaambia. Na walipokuwa wakimfungua mwanapunda, wenyewe waliwaambia, Mbona mnamfungua mwanapunda? Wakasema, Bwana anamhitaji. Wakampeleka kwa Yesu, wakatandika nguo zao juu ya mwanapunda, wakampandisha Yesu. Na alipokuwa akienda walitandaza nguo zao njiani. Na alipokuwa amekaribia mteremko wa mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo yote ya uwezo waliyoyaona, wakasema, Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu. Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako. Akajibu, akasema, Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatanena kwa sauti kuu.