Luka 22:54-62
Luka 22:54-62 SRUV
Wakamkamata, wakamchukua, wakaenda naye nyumbani kwa Kuhani Mkuu. Na Petro alimfuata kwa mbali. Na walipokwisha washa moto katikati ya kiwanja, waliketi pamoja, naye Petro akaketi kati yao. Ndipo mjakazi mmoja akamwona ameketi akiwa katika mwanga, akamkazia macho akasema, Na huyu alikuwa pamoja naye. Akakana, akisema, Ee mwanamke, simjui. Muda mfupi baadaye mtu mwingine alimwona akasema, Wewe nawe u mmoja wao. Petro akasema, Ee mtu, si mimi. Halafu, yapata saa moja, mtu mwingine alikazia akisema, Hakika na huyu alikuwa pamoja naye, kwa kuwa yeye pia ni Mgalilaya. Petro akasema, Ee mtu, sijui usemalo. Na papo hapo alipokuwa katika kusema, jogoo aliwika. Bwana akageuka akamtazama Petro. Petro akalikumbuka lile neno la Bwana jinsi alivyomwambia, Leo kabla hajawika jogoo utanikana mara tatu. Akatoka nje akalia kwa majonzi.