Mathayo 2:13-23
Mathayo 2:13-23 SRUV
Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hadi nitakapokuambia; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hadi Herode alipokufa; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nilimwita mwanangu. Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale majusi, alighadhibika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wa kiume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake kote, kuanzia wenye miaka miwili na chini yake, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale majusi. Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Sauti ilisikiwa Rama, Kilio na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, Asikubali kufarijiwa, kwa kuwa hawapo tena. Herode alipofariki, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri, akasema, Inuka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto. Akainuka akamchukua mtoto na mamaye, akaenda katika nchi ya Israeli. Lakini aliposikia ya kwamba Arkelao anatawala huko Yudea mahali pa Herode babaye, aliogopa kwenda huko; naye akiisha kuonywa katika ndoto, akaenda pande za Galilaya, akaenda, akakaa katika mji ulioitwa Nazareti; ili litimie neno lililonenwa na manabii, Ataitwa Mnazareti.