Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 8:23-34

Mathayo 8:23-34 SRUV

Akapanda katika mashua, wanafunzi wake wakamfuata. Kukawa na msukosuko mkuu baharini, hata mashua ikafunikwa na mawimbi; naye alikuwa amelala usingizi. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunaangamia. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu. Wale watu wakamaka wakisema, Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii? Naye alipofika ng'ambo, katika nchi ya Wagadara, watu wawili wenye pepo walikutana naye, wakitoka makaburini, wakali mno, hata mtu asiweze kuipitia njia ile. Na tazama, wakapiga kelele, wakisema, Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je! Umekuja kututesa kabla ya wakati wetu? Basi, kulikuwako mbali nao kundi la nguruwe wengi wakila. Wale pepo wakamsihi, wakisema, Ukitutoa, tuache twende, tukaingie katika lile kundi la nguruwe. Akawaambia, Nendeni. Wakatoka, wakaingia katika nguruwe; na kumbe! Kundi lote wakateremka kwa kasi gengeni hadi baharini, wakafa maji. Lakini wachungaji walikimbia, wakaenda zao mjini, wakazieneza habari zote na habari za wale wenye pepo pia. Na tazama, mji wote ukatoka kwenda kumlaki Yesu; nao walipomwona, walimsihi aondoke katika nchi yao.

Soma Mathayo 8