Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 9:18-31

Mathayo 9:18-31 SRUV

Alipokuwa akiwaambia hayo, tazama, akaja kiongozi mmoja, akamsujudia, akisema, Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi. Yesu Akaondoka, akamfuata, pamoja na wanafunzi wake. Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake. Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona. Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile. Yesu alipofika nyumbani kwa yule kiongozi, aliona wapiga filimbi, na makutano wakifanya maombolezo, akawaambia, Ondokeni; kwa maana msichana hakufa, amelala tu. Wakamcheka sana. Lakini makutano walipoondoshwa, aliingia, akamshika mkono; yule msichana akasimama. Habari hizi zikaenea katika nchi ile yote. Yesu alipokuwa akipita kutoka huko, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti, wakisema, Uturehemu, Mwana wa Daudi. Naye alipofika nyumbani, wale vipofu walimwendea; Yesu akawaambia, Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Wakamwambia, Naam, Bwana. Ndipo alipowagusa macho, akasema, Kwa kadiri ya imani yenu na itendeke kwenu. Macho yao yakafumbuka. Naye Yesu akawaagiza kwa nguvu, akisema, Angalieni hata mtu mmoja asijue. Lakini wakatoka, wakaeneza habari zake katika nchi ile yote.

Soma Mathayo 9