Marko 9:30-37
Marko 9:30-37 SRUV
Wakatoka huko, wakapita katikati ya Galilaya; naye hakutaka mtu kujua. Kwa sababu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake, akawaambia, Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua; na akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka. Lakini hawakulifahamu neno lile, wakaogopa kumwuliza. Wakafika Kapernaumu; hata alipokuwamo nyumbani, akawauliza, Mlishindania nini njiani? Wakanyamaza; kwa maana njiani walikuwa wakibishana wao kwa wao, ni nani aliye mkubwa. Akaketi chini, akawaita wale Kumi na Wawili akawaambia, Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote. Akatwaa kitoto, akamweka katikati yao, akamkumbatia, akawaambia, Mtu akimpokea mtoto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi; na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma.