Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 104

104
Mungu muumba na atoaye
1Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA.
Wewe, BWANA, Mungu wangu,
Umejifanya mkuu sana;
Umejivika heshima na utukufu.
2Umejivika nuru kama vazi;
Umezitandika mbingu kama pazia;
3 # Amo 9:6; Isa 19:1 Na kuziweka nguzo za ghorofa zake majini.
Huyafanya mawingu kuwa gari lake,
Na kwenda juu ya mabawa ya upepo,
4 # Ebr 1:7 Huwafanya malaika zake kuwa pepo,
Na watumishi wake kuwa moto wa miali.
5Uliiweka nchi juu ya misingi yake,
Isitikisike milele.
6Uliifunika kwa vilindi kama kwa vazi,
Maji yalikuwa yakisimama juu ya milima.
7Kwa kukemea kwako yakakimbia,
Kwa sauti ya radi yako yakaenda zake kasi,
8 # Ayu 38:10 Yakapanda milima, yakateremka mabondeni,
Mpaka mahali ulipoyatengenezea.
9 # Ayu 26:10; Zab 33:7; Yer 5:22; Mwa 9:11 Umeweka mpaka yasiupite,
Wala yasirudi kuifunikiza nchi.
10Hupeleka chemchemi katika mabonde;
Zapita kati ya milima;
11Zamnywesha kila mnyama wa porini;
Kwayo punda mwitu huzima kiu yao.
12Kandokando hukaa ndege wa angani;
Na kuimba wakiwa katika matawi.
13Huinywesha milima toka juu angani;
Nchi umeitosheleza kwa mazao ya kazi zako.
14 # Mwa 1:29,30; Zab 147:8; 136:25; Ayu 28:5 Huyameesha majani kwa makundi,
Na maboga kwa matumizi ya mwanadamu;
Ili atoe chakula katika nchi,
15 # Amu 9:13; Mit 31:6,7; Mhu 10:19; Yer 31:12; Mit 14:23; Yn 2:9,10 Na divai imfurahishe mtu moyo wake.
Aung'aze uso wake kwa mafuta,
Na mkate umburudishe mtu moyo wake.
16 # Hes 24:6; Zab 29:5 Miti ya BWANA nayo imetoshelezwa maji,
Mierezi ya Lebanoni aliyoipanda.
17Humo ndege hujenga viota vyao,
Korongo, anayo makao katika misonobari.
18 # Mit 30:26 Milima mirefu ndiko waliko mbuzi wa mwitu,
Na magenge ni kimbilio lao wibari.
19 # Mwa 1:14; Ayu 38:12 Aliufanya mwezi kwa ajili ya nyakati,
Jua latambua kuchwa kwake.
20 # Isa 45:7 Wewe hufanya giza, kukawa usiku,
Ndipo atambaapo kila mnyama wa mwitu.
21 # Ayu 38:39 Wanasimba hunguruma wakitaka mawindo,
Wakitafuta chakula chao kutoka kwa Mungu.
22Jua linapochomoza, wanakwenda zao,
Na kujilaza mapangoni mwao.
23 # Mwa 3:19 Mwanadamu atoka kwenda zake kazini,
Na kwenye utumishi wake mpaka jioni.
24 # Mwa 1:20-22 Ee BWANA, jinsi yalivyo mengi matendo yako!
Kwa hekima umevifanya vyote pia.
Dunia imejaa viumbe wako.
25Bahari iko kule, kubwa na upana,
Ndimo mlimo viendavyo visivyohesabika,
Viumbe hai wakubwa kwa wadogo.
26 # Ayu 41:1; Zab 74:14; Isa 27:1 Ndimo zipitamo merikebu,
Ndimo alimo Lewiathani uliyemwumba acheze humo.
27 # Rum 11:36 Hao wote wanakungoja Wewe,
Uwape chakula chao kwa wakati wake.
28Wewe huwapa,
Wao wanakiokota;
Wewe waukunjua mkono wako,
Wao wanashiba mema;
29 # Mhu 12:7 Wewe wauficha uso wako,
Wao wanafadhaika;
Waiondoa pumzi yao, wanakufa,
Na kuyarudia mavumbi yao,
30 # Isa 32:15 Waituma roho yako, wanaumbwa,
Nawe waufanya upya uso wa nchi.
31Utukufu wa BWANA na udumu milele;
BWANA na ayafurahie matendo yake.
32 # Hab 3:10 Aitazamaye nchi, ikatetemeka;
Aigusaye milima, ikatoka moshi.
33Nitamwimbia BWANA maadamu ninaishi;
Nitamshangilia Mungu wangu nikiwa hai;
34Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake;
Maana furaha yangu hutoka kwa BWANA.
35 # Mit 2:22 Wenye dhambi waangamizwe katika nchi,
Watendao ubaya wasiwepo tena.
Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA.

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 104: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia