Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 12

12
Mungu anamwita Abramu aiache nchi yake
1Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Abramu, “Ondoka katika nchi yako, acha jamaa yako na nyumba ya baba yako, uende katika nchi nitakayokuonesha. 2Nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, nitakubariki na kulikuza jina lako, nawe uwe baraka.#12:2 Ahadi ya Mungu kwa Abrahamu ni kiungo muhimu kinachoshikilia umoja wa historia yote ya mababu wa Waisraeli ambayo inasimuliwa katika kitabu cha Mwanzo. Katika sura zinazofuata, ahadi hiyo itarudiwa mara kwa mara kwa kutaja viini vyake muhimu: ahadi ya kuwa na wazawa wengi (Mwa 13:16; 15:5; 17:6; 22:17-18; 26:4;28:14) na ahadi ya kuimiliki nchi ambapo Abrahamu, Isaka na Yakobo waliishi kama wageni (Mwa 15:18-21; 26:3; 28:15; 50:24).
3Anayekubariki, nitambariki;
anayekulaani, nitamlaani.
Kwako wewe, nitayabariki#12:2-3 Katika aya hizi mbili neno “baraka”, bariki n.k. linatumika mara tano, jambo ambalo linaonesha umuhimu wake. Baraka aliyoahidiwa Abrahamu na kwa kupitia kwake watu wa Israeli hata kufikia binadamu wote inachukua nafasi ya laana iliyowapata binadamu wote kwa sababu ya dhambi (Mwa 3:17; rejea 4:11; 5:29; 8:21; 9:25). Rejea Gal 3:6-14. mataifa yote ya dunia.”#12:3 Rejea Mate 3:25; Gal 3:8; taz pia Mwa 18:18; 22:18; 26:4; 28:14. Tafsiri nyingine yamkini kwa aya 3b ni: “watu wote duniani watabarikiwa kama wewe ulivyobarikiwa”.
4Kwa hiyo, Abramu akaondoka kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru;#12:4 Abramu akaondoka kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru: A.J. linachukua jambo hilo la kutii mara moja agizo la Mungu kuwa kitendo maalumu na hivyo kumwona Abrahamu kuwa babu na mfano wa wote wanaomwamini Yesu Kristo (rejea Rom 4:11-12; Gal 4:6-7; Ebr 11:8-10). na Loti akaenda pamoja naye. Abramu alikuwa na umri wa miaka 75 alipotoka Harani. 5Alimchukua Sarai mkewe, na Loti mwana wa ndugu yake, pamoja na mali yao yote na watu wote waliokuwa wamejipatia huko Harani, wakaondoka kuelekea nchi ya Kanaani. Walipoingia nchini Kanaani, 6Abramu akapita katikati ya nchi mpaka Shekemu,#12:6 Shekemu: Mji wa zamani wa Palestina ulioko kati ya Mlima Ebali na Mlima Gerizimu (taz Kumb 11:29-30 maelezo). Kabla ya Waisraeli kuuteka, mji huo ulikuwa maarufu kama kituo muhimu cha kidini cha watu wa Kanaani. mahali patakatifu, penye mti wa mwaloni wa More.#12:6 Mwaloni wa More: Huo ulikuwa mti au pengine kichaka au msitu mdogo ambao ulitumika kama mahali pa ibada (rejea Mwa 35:4; Yos 24:26). Yawezekana pia kwamba ni mti ule ule ambao katika Amu 9:37 unaitwa Mwaloni wa “Waaguzi”. Wakati huo, Wakanaani walikuwa ndio wenyeji wa nchi hiyo. 7Ndipo Mwenyezi-Mungu akamtokea Abramu, akamwambia, “Wazawa wako nitawapa nchi hii.” Basi, Abramu akajenga madhabahu kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu aliyemtokea. 8Baadaye Abramu akaondoka, akaelekea mlimani mashariki ya Betheli akapiga hema kati ya mji wa Betheli,#12:8 Betheli: Jina ambalo katika Kiebrania lina maana ya “Nyumba ya Mungu” (Mwa 28:17,19); huo ulikuwa pia kituo maarufu cha kidini kwa Wakanaani, yapata kilomita 15 kaskazini ya Yerusalemu. Wakati wa tawala mbili za Waisraeli, Betheli ulikuwa mji muhimu kwa utawala wa kaskazini wa Israeli maana hapo kulikuwa na mahali pakuu pa ibada kwa ajili ya ufalme wa kaskazini (1Fal 12:28-30; Amo 7:13). upande wa magharibi, na mji wa Ai upande wa mashariki. Hapo pia akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu na kumwomba kwa jina lake. 9Kisha Abramu akaendelea kusafiri kuelekea upande wa Negebu.#12:9 Negebu: Eneo lililoko kusini mwa Palestina ambako kwa kawaida ni jangwa. Jina lenyewe katika Kiebrania lina maana ya “Kusini”. Maneno “akaendelea kusafiri” yanajaribu kutoa picha ile ya safari za mabedui jangwani pamoja na mahema yao.
Abramu nchini Misri
10Wakati huo, njaa ilitokea nchini.#12:10 Njaa ilitokea nchini: Huko Palestina daima mavuno yalitegemea sana mvua (rejea Kumb 11:10-12). A.K. linataja mara kwa mara matukio ya njaa kwa sababu ya ukame wa muda mrefu (Mwa 26:1; 43:1; 47:4; Rut 1:1; 2Fal 4:38). Njaa hiyo ilikuwa kali, hivyo Abramu akalazimika kwenda Misri#12:10 Abramu akalazimika kwenda Misri: Huko Misri (Afrika ya kaskazini) nyakati hizo mavuno yalitokea kila msimu wake, tena bila kukosekana kwa vile mafuriko ya mto Nili yaliimwagilia maji ardhi iliyolimwa. Hati za kale za Kimisri zinathibitisha kwamba kulipotokea njaa huko nchini Kanaani wageni wengi walitiririkia nchini Misri kununua nafaka na mara nyingine baadhi yao wakabaki huko kama wakimbizi. Rejea Mwa 41:3-4. kukaa huko kwa muda. 11Alipokaribia Misri, Abramu alimwambia Sarai mkewe, “Najua kuwa wewe ni mwanamke mzuri na wa kuvutia. 12Wamisri watakapokuona watasema, ‘Huyu ni mkewe,’ kisha wataniua lakini wewe watakuacha hai. 13Basi, waambie kuwa wewe ni dada yangu#12:13 Wewe ni dada yangu: Taz Mwa 26:6-11 ambapo Isaka naye pia anasema hivyo kuhusu mkewe Rebeka. Kama inavyodhihirika katika sura 20:12 Sara alikuwa dada wa kambo wa Abrahamu. Wengine wanaona hapa desturi iliyokuwa kule Harani alikotoka Abrahamu, desturi ambayo mume aliweza kumchukua mkewe na kumtangaza rasmi kuwa ni dada yake na hivyo kumpa hadhi fulani au cheo maalumu na kinga katika jamii. ili mambo yaniendee vema, niachwe niishi kwa ajili yako.” 14Basi, Abramu alipowasili nchini Misri, wenyeji wa huko walimwona Sarai kuwa ni mwanamke mzuri sana. 15Maofisa wa Farao walipomwona Sarai, wakamsifia kwa Farao. Basi, Sarai akapelekwa nyumbani kwa Farao.#12:15 Farao: Taz Kut 1:11 maelezo. 16Basi, kwa ajili yake, Farao alimfadhili Abramu, akampa kondoo, ng'ombe, punda dume, watumishi wa kiume na wa kike, punda jike na ngamia.
17Lakini Mwenyezi-Mungu akamtesa Farao na watu wote wa nyumba yake kwa mapigo makali kwa sababu ya Sarai, mkewe Abramu. 18Farao akamwita Abramu, akamwuliza, “Ni kitu gani hiki ulichonitendea? Mbona hukunijulisha kwamba Sarai ni mkeo?#12:18 Aya hii haisemi jinsi Farao alivyogundua kuwa Sarai alikuwa mke wa Abrahamu. 19Kwa nini ulisema ni dada yako hata nikamchukua kuwa mke wangu? Basi, sasa mkeo ndiye huyo. Mchukue uende zako!” 20Kisha Farao aliwaamuru watu wake, nao wakamsindikiza Abramu njiani akiwa na mke wake na mali yake yote.

Iliyochaguliwa sasa

Mwanzo 12: BHNTLK

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia