Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 18

18
Yesu Akamatwa
(Mt 26:47-56; Mk 14:43-50; Lk 22:47-53)
1Yesu alipomaliza kuomba, akaondoka pamoja na wafuasi wake kwenda ng'ambo kuvuka bonde la Kidroni. Akaenda katika bustani mahali hapo, akiwa bado pamoja na wafuasi wake.
2Yuda, yule aliyehusika kumsaliti Yesu, alipafahamu mahali pale. Alipajua kwa sababu Yesu mara nyingi alikutana na wafuasi wake pale. 3Kwa hiyo Yuda akaongoza kundi la askari hadi katika bustani hiyo pamoja na walinzi wengine kutoka kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo. Hawa walikuwa wamebeba mienge, taa, na silaha.
4Yesu alikwisha kujua yote ambayo yangempata. Hivyo aliwaendea na kuwauliza, “Je! ni nani mnayemtafuta?”
5Wakamjibu, “Yesu kutoka Nazareti.”
Akawaambia, “Mimi ni Yesu.”#18:5 Mimi ni Yesu Kwa maana ya kawaida, “Mimi ndimi”, ambayo inaweza kuwa na maana ile ile hapa kama ilivyo katika 8:24,28,58; 13:19. Pia katika mstari wa 8. (Yuda yule aliyehusika kumsaliti Yesu alikuwa amesimama hapo pamoja nao.) 6Yesu aliposema, “Mimi ni Yesu,” wale watu walirudi nyuma na kuanguka chini.
7Akawauliza tena, “Je! ni nani mnayemtafuta?”
Wakasema, “Yesu kutoka Nazareti.”
8Yesu akasema, “Nimewaambia kwamba mimi ndiye Yesu. Hivyo kama mnanitafuta mimi, basi waacheni huru watu hawa waende zao.” 9Hii ilikuwa kuonesha ukweli wa yale aliyosema Yesu mapema: “Sikumpoteza hata mmoja wa wale ulionipa.”
10Simoni Petro akauchomoa upanga aliokuwa ameufunga kiunoni. Akampiga nao mtumishi wa Kuhani Mkuu, na kulikata sikio lake la kulia. (Jina la mtumishi huyo lilikuwa ni Maliko.) 11Yesu akamwambia Petro, “Rudisha jambia lako mahali pake! Ninapaswa kunywa toka kikombe#18:11 kikombe Kikombe ni ishara ya mateso. Yesu alitumia dhana ya kukinywea kikombe akimaanisha kuyakubali mateso ambayo angeyapata katika matukio ya kutisha ambayo yangetokea muda mfupi ujao. ambacho Baba amenipa nikinywee.”
Yesu Aletwa Mbele ya Anasi
(Mt 26:57-58; Mk 14:53-54; Lk 22:54)
12Kisha askari hao pamoja na mkuu wao na walinzi wa Kiyahudi wakamkamata Yesu. Wakamfunga, 13nao wakampeleka kwanza kwa Anasi, baba mkwe wa Kayafa. Kayafa alikuwa Kuhani Mkuu kwa mwaka huo. 14Naye ndiye aliyewashauri viongozi wengine wa Kiyahudi kwamba ingemfaa mtu mmoja afe#18:14 mtu mmoja afe Kifo cha Yesu kilikuwa kwa ajili ya watu wote wa ulimwengu siyo kwa Wayahudi peke yao. kwa ajili ya watu wote.
Petro Amkana Yesu
(Mt 26:69-70; Mk 14:66-68; Lk 22:55-57)
15Simoni Petro na mmoja wa wafuasi wengine wa Yesu walienda pamoja na Yesu. Mfuasi huyu alimfahamu kuhani mkuu. Hivyo akaingia pamoja na Yesu ndani ya uwanja wa nyumba ya kuhani mkuu. 16Lakini Petro alisubiri nje karibu na mlango. Yule mfuasi aliyemjua kuhani mkuu alirudi nje na kuongea na mlinda mlango. Kisha alimleta Petro ndani. 17Msichana aliyekuwepo langoni alimwambia Petro, “Je! Wewe pia ni mmoja wa wafuasi wa mtu yule?”
Petro akajibu, “Hapana, mimi siye!”
18Ilikuwa baridi, hivyo watumishi na walinzi waliwasha moto wa kuni. Walikuwa wameuzunguka, wakipasha joto miili yao naye Petro alikuwa amesimama pamoja nao.
Kuhani Mkuu Amhoji Yesu
(Mt 26:59-66; Mk 14:55-64; Lk 22:66-71)
19Kuhani Mkuu akamwuliza Yesu maswali kuhusu wafuasi wake pamoja na mafundisho aliyowapa. 20Yesu akamjibu, “Daima nimesema wazi kwa watu wote. Siku zote nimefundisha kwenye masinagogi na kwenye eneo la Hekalu. Wayahudi wote hukusanyika pale. Sijawahi kusema jambo lo lote kwa siri. 21Sasa kwa nini unaniuliza? Waulize watu waliosikia mafundisho yangu. Wao wanajua niliyosema!”
22Yesu aliposema hivyo, mmoja wa walinzi aliyekuwa amesimama hapo akampiga. Mlinzi huyo akasema, “Hupaswi kusema hivyo kwa kuhani mkuu!”
23Yesu akajibu, “Kama nimesema vibaya jambo lo lote, mwambie kila mtu hapa kosa lenyewe. Lakini kama niliyosema ni sahihi, kwa nini basi unanipiga?”
24Hivyo Anasi akampeleka Yesu kwa Kayafa kuhani mkuu. Naye alikuwa bado amefungwa.
Petro Amkana Yesu tena
(Mt 26:71-75; Mk 14:69-72; Lk 22:58-62)
25Simoni Petro alikuwa amesimama karibu na moto, akijipasha joto. Watu wengine wakamwambia Petro, “Je! wewe si mmoja wa wafuasi wa mtu yule?”
Petro alikataa hilo. Akasema, “Hapana, mimi siye.”
26Mmoja wa watumishi wa kuhani mkuu alikuwapo pale. Naye alikuwa ni jamaa wa mtu yule aliyekatwa sikio na Petro. Mtumishi akamwambia Petro, “Nadhani nilikuona pamoja naye pale kwenye bustani!”
27Lakini kwa mara nyingine Petro akasema, “Hapana, sikuwa pamoja naye!” Mara tu alipomaliza kusema hayo, jogoo akawika.
Yesu Apelekwa kwa Gavana Pilato
(Mt 27:1-2,11-31; Mk 15:1-20; Lk 23:1-25)
28Kisha walinzi wakamchukua Yesu kutoka katika nyumba ya Kayafa kwenda kwenye jumba la mtawala wa Kirumi. Nayo ilikuwa ni mapema asubuhi. Wayahudi waliokuwa pale wasingeweza kuingia ndani ya jumba hilo. Wao hawakutaka kujinajisi wenyewe kwa sababu walitaka kuila karamu ya Pasaka. 29Kwa hiyo Pilato akatoka nje kuwafuata na akawauliza, “Mnasema mtu huyu amefanya makosa gani?”
30Wakajibu, “Yeye ni mtu mbaya. Ndiyo maana tumemleta kwako.”
31Pilato akawaambia, “Mchukueni wenyewe na kumhukumu kufuatana na sheria yenu.” Viongozi wa Wayahudi wakamwambia, “Lakini sheria yako haituruhusu sisi kumwadhibu mtu yeyote kwa kumwua.” 32(Hii ilikuwa ni kuonesha ukweli wa yale aliyosema Yesu juu ya jinsi ambavyo angekufa.)
33Kisha Pilato alirudi ndani ya jumba lile. Aliagiza Yesu aje na akamuuliza, “Je! wewe ni Mfalme wa Wayahudi?”
34Yesu akajibu, “Je! hilo ni swali lako mwenyewe au watu wengine wamekuambia juu yangu?”
35Pilato akajibu, “Mimi sio Myahudi! Ni watu wako mwenyewe na viongozi wa makuhani waliokuleta kwangu. Je! umefanya kosa gani?”
36Yesu akajibu, “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ungekuwa hivyo, watumishi wangu wangenipigania ili nisikabidhiwe kwa viongozi wa Wayahudi. Hapana, ufalme wangu sio wa kidunia.”
37Pilato akasema, “Kwa hiyo wewe ni mfalme?”
Yesu akamjibu, “Uko sahihi unaposema kuwa mimi ni mfalme. Nami nilizaliwa kwa ajili ya hili: kuwaeleza watu juu ya kweli. Ni kwa sababu hii nalikuja ulimwenguni. Kila mmoja aliye wa upande wa kweli hunisikiliza.”
38Pilato akasema, “Kweli ndiyo nini?” Kisha alitoka nje tena kwenda kwa viongozi wa Wayahudi na kuwaimbia, “Mimi sipati kitu chochote kibaya cha kumpinga mtu huyu. 39Lakini ni moja ya desturi zenu kwangu mimi kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa Pasaka. Je! mnataka niwafungulie huyu ‘Mfalme wa Wayahudi’?”
40Wakajibu kwa kupiga kelele wakisema, “Hapana, siyo yeye! Mwache huru Baraba!” (Baraba alikuwa jambazi.)

Iliyochaguliwa sasa

Yohana 18: TKU

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia