20
Ibrahimu na Abimeleki
1Basi Ibrahimu akaondoka huko akaenda hadi nchi ya Negebu, akaishi kati ya Kadeshi na Shuri. Kwa muda mfupi alikaa Gerari. 2Huko Ibrahimu akasema kuhusu Sara mkewe, “Huyu ni dada yangu.” Kisha Abimeleki mfalme wa Gerari akaagiza Sara aletwe, naye akamchukua awe mkewe.
3Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto usiku na kumwambia, “Wewe ni kama mfu kwa sababu ya huyu mwanamke uliyemchukua; yeye ni mke wa mtu.”
4Wakati huo Abimeleki alikuwa bado hajamsogelea, kwa hiyo akasema, “Je, Bwana utaliharibu taifa lisilo na hatia? 5Hakusema kwangu, ‘Huyu ni dada yangu’; naye Sara pia hakusema, ‘Huyu ni kaka yangu’? Nimefanya haya kwa dhamiri safi na mikono safi.”
6Kisha Mungu akamwambia katika ndoto ile, “Ndiyo, najua kwamba umefanya haya kwa dhamiri safi, kwa hiyo nimekuzuia usinitende dhambi. Ndiyo sababu sikukuacha umguse. 7Sasa umrudishe huyo mke wa mtu, kwa maana ni nabii, naye atakuombea nawe utaishi. Lakini kama hutamrudisha, ujue kwa hakika kuwa wewe na watu wako wote mtakufa.”
8Kesho yake asubuhi na mapema, Abimeleki akawaita maafisa wake wote, na baada ya kuwaambia yote yaliyotukia, waliogopa sana. 9Kisha Abimeleki akamwita Ibrahimu na kumwambia, “Wewe umetufanyia nini? Nimekukosea nini hata ukaleta hatia kubwa namna hii kwangu na kwa ufalme wangu? Umenifanyia mambo ambayo hayakupasa kufanyika.” 10Abimeleki akamuuliza Ibrahimu, “Ulikuwa na kusudi gani kufanya hivi?”
11Ibrahimu akajibu, “Niliwaza kwamba, ‘Hakika hakuna hofu ya Mungu mahali hapa, nao wataniua kwa sababu ya mke wangu.’ 12Pamoja na hayo, ni kweli kwamba yeye ni dada yangu, binti ya baba yangu ingawa si mtoto wa mama yangu; basi akawa mke wangu. 13Mungu aliponifanya nisafiri mbali na nyumbani mwa baba yangu, nilimwambia, ‘Hivi ndivyo utakavyoonesha pendo lako kwangu: Kila mahali tutakapoenda, sema hivi kunihusu, “Huyu ni kaka yangu.” ’ ”
14Kisha Abimeleki akatwaa kondoo na ng’ombe, na watumwa wa kiume na wa kike, akampa Ibrahimu, na akamrudisha Sara kwa mumewe. 15Abimeleki akasema, “Nchi yangu iko mbele yako; ishi popote unapotaka.”
16Akamwambia Sara, “Ninampa kaka yako shekeli elfu moja za fedha. Hii ni kufidia kosa lililofanyika dhidi yako mbele ya wote walio pamoja nawe; haki yako imethibitishwa kabisa.”
17Kisha Ibrahimu akamwomba Mungu, naye Mungu akamponya Abimeleki, mke wake, na wajakazi wake ili waweze kupata watoto tena, 18kwa kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa amefunga tumbo za wanawake wote wa nyumba ya Abimeleki kwa sababu ya Sara, mke wa Ibrahimu.