15
Isa mzabibu wa kweli
1“Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. 2Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda, Baba yangu hulikata, nalo kila tawi linalozaa, hulisafisha ili lipate kuzaa matunda zaidi. 3Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililonena nanyi. 4Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa matunda lisipokaa ndani ya mzabibu, vivyo hivyo ninyi msipokaa ndani yangu hamwezi kuzaa matunda.
5“Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya jambo lolote. 6Mtu yeyote asipokaa ndani yangu, huyo hutupwa nje kama tawi na kunyauka. Matawi kama hayo hukusanywa na kutupwa motoni, yakateketea. 7Mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lolote mtakalo, nanyi mtatendewa. 8Kwa hiyo Baba yangu hutukuzwa kwa vile mnavyozaa matunda mengi, nanyi mtajidhihirisha kuwa wanafunzi wangu.
9“Kama vile Baba alivyonipenda mimi, hivyo ndivyo mimi nilivyowapenda ninyi. Basi kaeni katika pendo langu. 10Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. 11Nimewaambia mambo haya ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu iwe kamili. 12Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi. 13Hakuna mtu mwenye upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. 14Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru. 15Siwaiti ninyi watumishi tena, kwa sababu watumishi hawajui bwana wao analofanya. Bali nimewaita ninyi rafiki, kwa maana nimewajulisha mambo yote niliyoyasikia kutoka kwa Baba yangu. 16Si ninyi mlionichagua, bali mimi ndiye niliyewachagua ninyi na kuwaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kudumu. Ili nalo lolote mtakalomwomba Baba katika Jina langu, awape ninyi. 17Amri yangu ndiyo hii: Mpendane.
Ulimwengu wawachukia wanafunzi
18“Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba ulinichukia mimi kabla yenu. 19Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda kama unavyowapenda walio wake. Kwa sababu ninyi si wa ulimwengu, lakini mimi nimewachagua kutoka ulimwengu, hii ndiyo sababu ulimwengu unawachukia. 20Kumbukeni lile neno nililowaambia, ‘Hakuna mtumishi aliye mkuu kuliko bwana wake.’#15:20 Yohana 13:16 Kama wamenitesa mimi, nanyi pia watawatesa. Kama wamelishika neno langu, watalishika na neno lenu pia. 21Watawatendea ninyi haya yote kwa ajili ya Jina langu, kwa sababu hawamjui yeye aliyenituma. 22Kama sikuja na kusema nao, hawangekuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa hawana udhuru kwa ajili ya dhambi zao. 23Yeyote anayenichukia mimi, anamchukia pia na Baba yangu. 24Kama sikuwa nimefanya miujiza ambayo haijapata kufanywa na mtu mwingine yeyote, hawangekuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa wameiona miujiza hii, na bado wakatuchukia mimi na Baba yangu. 25Lakini hii ni kutimiza lile neno lililoandikwa kwenye Torati kwamba, ‘Walinichukia pasipo sababu.’#15:25 Zaburi 35:19; 69:4
Kazi ya Roho Mtakatifu wa Mungu
26“Lakini atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu kutoka kwa Baba, yaani huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi. 27Ninyi nanyi itawapasa kushuhudia kwa sababu mmekuwa pamoja nami tangu mwanzo.