20
Isa afufuka
(Mathayo 28:1-8; Marko 16:1-8; Luka 24:1-12)
1Alfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma, kulipokuwa bado giza, Mariamu Magdalene alienda kaburini na kukuta lile jiwe limeondolewa penye ingilio. 2Hivyo akakimbia kwa Simoni Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine ambaye Isa alimpenda, na kusema, “Wamemwondoa Bwana kaburini, na hatujui walikomweka!”
3Petro na yule mwanafunzi mwingine wakaondoka mara moja kuelekea kaburini. 4Wote wawili walikuwa wanakimbia, lakini yule mwanafunzi mwingine akakimbia mbio kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini. 5Akainama na kuchungulia mle kaburini, akaona vile vitambaa vya kitani, lakini hakuingia. 6Ndipo Simoni Petro akaja akimfuata nyuma, akaingia ndani ya kaburi. Naye akaona vile vitambaa vya ile sanda vikiwa pale chini, 7na kile kitambaa kilichokuwa kichwani mwa Isa. Kitambaa hicho kilikuwa kimekunjwa peke yake, mbali na vile vitambaa vya kitani vya ile sanda. 8Kisha yule mwanafunzi aliyetangulia kufika kaburini akaingia ndani, akaona, na akaamini. 9(Kwa kuwa hadi wakati huo walikuwa bado hawajaelewa kutoka Maandiko kwamba ilikuwa lazima Isa afufuke kutoka kwa wafu.)
10Kisha hao wanafunzi wakaondoka, wakarudi nyumbani mwao.
Isa aonekana baada ya kufufuka
(Yohana 20:11–21:25)
Isa amtokea Mariamu Magdalene
(Mathayo 28:9-10; Marko 16:9-11)
11Lakini Mariamu Magdalene akasimama nje ya kaburi akilia. Alipokuwa akilia, akainama kuchungulia mle kaburini, 12naye akaona malaika wawili wamevaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Isa ulipokuwa umelazwa, mmoja upande wa kichwani na mwingine upande wa miguuni.
13Wakamuuliza Mariamu, “Mwanamke, mbona unalia?”
Akawaambia, “Nalia kwa kuwa wamemchukua Bwana wangu, na sijui walikomweka.” 14Baada ya kusema hayo, akageuka, akamwona Isa amesimama, lakini hakumtambua.
15Isa akamwambia, “Mwanamke, mbona unalia? Unamtafuta nani?”
Mariamu, akidhani alikuwa anaongea na mtunza bustani, akamwambia, “Bwana, kama ni wewe umemchukua, tafadhali nioneshe ulikomweka, nami nitamchukua.”
16Isa akamwita, “Mariamu!”
Ndipo Mariamu akamgeukia Isa na kusema naye kwa Kiebrania, “Raboni!” (maana yake “Mwalimu”).
17Isa akamwambia, “Usinishike, kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba#20:17 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili.. Lakini nenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ‘Ninapaa kwenda kwa Baba yangu ambaye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu ambaye ni Mungu wenu.’ ”
18Kwa hiyo Mariamu Magdalene akaenda kuwatangazia wanafunzi wa Isa, akisema, “Nimemwona Bwana!” Naye akawaambia kwamba Isa alikuwa amemweleza mambo hayo yote.
Isa awatokea wanafunzi wake
(Mathayo 28:16-20; Marko 16:14-18; Luka 24:36-49)
19Ilipokuwa jioni ya siku hiyo hiyo ya kwanza ya juma, wanafunzi wake walikuwa pamoja, milango ikiwa imefungwa kwa kuwaogopa viongozi wa Wayahudi. Naye Isa akawatokea, akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi!” 20Baada ya kusema haya, akawaonesha mikono yake na ubavu wake. Wanafunzi wake wakafurahi sana walipomwona Bwana Isa.
21Isa akawaambia tena, “Amani iwe nanyi! Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami nawatuma ninyi.” 22Alipokwisha kusema haya, akawavuvia, akawaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu wa Mungu. 23Mkimwondolea mtu yeyote dhambi zake, zitaondolewa; na yeyote msiyemwondolea dhambi zake, hazitaondolewa.”
Isa amtokea Tomaso
24Lakini Tomaso (aliyeitwa Didimasi#20:24 yaani Pacha), mmoja wa wale kumi na wawili, hakuwa pamoja nao Isa alipokuja. 25Hivyo wale wanafunzi wengine wakamwambia, “Tumemwona Bwana Isa.”
Lakini yeye akawaambia, “Nisipoona zile alama za misumari mikononi mwake, na kuweka kidole changu kwenye hizo alama za misumari, na mkono wangu ubavuni mwake, sitaamini.”
26Baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwa tena pamoja ndani ya nyumba, naye Tomaso alikuwa pamoja nao. Ndipo Isa akaja, milango ikiwa imefungwa, na kusimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi.” 27Kisha akamwambia Tomaso, “Weka kidole chako hapa na uone mikono yangu, nyoosha mkono wako uguse ubavuni mwangu. Usiwe na shaka, bali uamini tu.”
28Tomaso akamwambia, “Bwana wangu na Mungu wangu!”
29Isa akamwambia, “Umeamini kwa kuwa umeniona? Wamebarikiwa wale ambao hawajaona lakini wameamini.”
Kusudi la kitabu hiki
30Isa alifanya miujiza mingine mingi mbele za wanafunzi wake, ambayo haikuandikwa katika kitabu hiki. 31Lakini hii imeandikwa ili mweze kuamini ya kuwa Isa ndiye Al-Masihi#20:31 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta., Mwana wa Mungu, na kwa kumwamini mpate uzima katika jina lake.