9
Isa awatuma wale kumi na wawili
(Mathayo 10:5-15; Marko 6:7-13)
1Isa kisha akawaita wale kumi na wawili pamoja, akawapa mamlaka na uwezo wa kutoa pepo wachafu wote na kuponya magonjwa yote, 2kisha akawatuma waende wakahubiri ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa. 3Akawaagiza akisema, “Msichukue chochote safarini: sio fimbo, wala mkoba, wala mkate, wala fedha, hata msichukue kanzu ya ziada. 4Katika nyumba yoyote mwingiayo, kaeni humo hadi mtakapoondoka katika mji huo. 5Kama watu wasipowakaribisha, mnapoondoka katika mji wao, kung’uteni mavumbi kutoka miguu yenu ili kuwa ushuhuda dhidi yao.” 6Hivyo wale wanafunzi wakaondoka wakaenda kutoka kijiji hadi kijiji, wakihubiri habari njema na kuponya wagonjwa kila mahali.
Herode afadhaika
(Mathayo 14:1-12; Marko 6:14-29)
7Basi Mfalme Herode, mtawala wa Galilaya, alisikia habari za yote yaliyotendeka. Naye akafadhaika, kwa kuwa baadhi ya watu walikuwa wakisema Yahya amefufuliwa kutoka kwa wafu. 8Wengine wakasema Ilya amewatokea, na wengine kwamba mmoja wa manabii wa kale amefufuka. 9Herode akasema, “Yahya nilimkata kichwa. Lakini ni nani huyu ninayesikia mambo kama haya kumhusu?” Akatamani sana kumwona.
Isa alisha wanaume 5,000
(Mathayo 14:13-21; Marko 6:30-44; Yohana 6:1-14)
10Mitume wake waliporudi, wakamweleza Isa yote waliyofanya. Kisha akaenda nao faraghani hadi mji uitwao Bethsaida. 11Lakini umati wa watu wakafahamu alikoenda, wakamfuata. Akawakaribisha na kunena nao kuhusu ufalme wa Mungu na kuwaponya wale wote waliokuwa wanahitaji uponyaji.
12Ilipokaribia jioni, wale mitume kumi na wawili wakaenda kwa Isa na kumwambia, “Waage watu hawa ili waende vijijini jirani na mashambani, ili wapate chakula na mahali pa kulala, kwa maana hapa tuko nyikani.”
13Isa akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.”
Nao wakajibu, “Tuna mikate mitano na samaki wawili tu. Labda twende tukanunue chakula cha kuwatosha watu hawa wote.” 14(Walikuwepo wanaume wapatao elfu tano.)
Isa akawaambia wanafunzi wake, “Waketisheni katika vikundi vya watu hamsini hamsini.” 15Wanafunzi wakafanya hivyo, wakawaketisha wote. 16Isa akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akavibariki na kuvimega. Kisha akawapa wanafunzi ili wawagawie watu. 17Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili.
Petro amkiri Isa kuwa Al-Masihi
(Mathayo 16:13-19; Marko 8:27-29)
18Siku moja Isa alipokuwa akiomba faraghani, nao wanafunzi wake wakiwa pamoja naye, akawauliza, “Watu husema mimi ni nani?”
19Wakamjibu, “Baadhi husema wewe ni Yahya, wengine husema ni Ilya, na wengine husema kwamba ni mmoja wa manabii wa kale amefufuka.”
20Kisha akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?”
Petro akajibu, “Wewe ndiwe Al-Masihi#9:20 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta. wa Mungu.”
21Isa akawakataza wasimwambie mtu yeyote jambo hilo.
Isa atabiri kifo chake
(Mathayo 16:21-28; Marko 8:31–9:1)
22Isa akasema, “Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi na kukataliwa na wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa Torati, na itampasa auawe, lakini siku ya tatu kufufuliwa kutoka mauti.”
23Kisha akawaambia wote, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake kila siku, anifuate. 24Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayaokoa. 25Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akapoteza au kuangamiza nafsi yake? 26Mtu yeyote akinionea aibu mimi na maneno yangu, Mwana wa Adamu naye atamwonea aibu atakapokuja katika utukufu wake na katika utukufu wa Baba#9:26 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu., pamoja na malaika watakatifu.
27“Amin, nawaambia, wako baadhi ya watu waliosimama hapa ambao hawataonja mauti kabla ya kuuona ufalme wa Mungu.”
Isa abadilika sura
(Mathayo 17:1-8; Marko 9:2-8)
28Yapata siku nane baada ya Isa kusema hayo, aliwachukua Petro, Yohana na Yakobo, akaenda nao mlimani kuomba. 29Alipokuwa akiomba, sura ya uso wake ikabadilika, nayo mavazi yake yakametameta kama miali ya radi. 30Ghafula wakawaona watu wawili, ndio Musa na Ilya, wakizungumza naye. 31Walionekana katika utukufu wakizungumza na Isa kuhusu kifo chake ambacho kingetokea huko Yerusalemu. 32Petro na wenzake walikuwa wamelala usingizi mzito. Walipoamka, wakaona utukufu wa Isa na wale watu wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye. 33Musa na Ilya walipokuwa wanaondoka, Petro akamwambia Isa, “Bwana, ni vizuri tukae hapa! Tutajenga vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Musa na kingine cha Ilya.” Lakini Petro hakujua alichosema.
34Alipokuwa bado anazungumza, pakatokea wingu, likawafunika, nao wakaogopa walipoingia mle kwenye wingu. 35Sauti ikatoka kwenye lile wingu ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, niliyemchagua. Msikieni yeye.” 36Baada ya sauti hiyo kusema, walimkuta Isa akiwa peke yake. Wale wanafunzi wakalihifadhi jambo hili, wala kwa wakati huo hawakumwambia mtu yeyote yale waliyokuwa wameyaona.
Isa amponya kijana mwenye pepo mchafu
(Mathayo 17:14-21; Marko 9:14-29)
37Kesho yake waliposhuka kutoka mlimani, alikutana na umati mkubwa wa watu. 38Mtu mmoja katika umati ule akapaza sauti, akasema, “Mwalimu, naomba umwangalie mwanangu, kwani ndiye mtoto wangu wa pekee. 39Mara kwa mara pepo mchafu humpagaa na kumfanya apige mayowe, kisha humwangusha na kumtia kifafa hata akatokwa na povu kinywani. Huyo pepo mchafu anamtesa sana, na hamwachi ila mara chache. 40Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.”
41Isa akawajibu, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka! Nitakaa nanyi na kuwavumilia hadi lini? Mlete mwanao hapa.”
42Hata yule mtoto alipokuwa akija, yule pepo mchafu akamwangusha, akamtia kifafa. Lakini Isa akamkemea yule pepo mchafu amtoke, akamponya yule mtoto, na akamrudisha kwa baba yake. 43Watu wote wakastaajabia uweza mkuu wa Mungu.
Wakati bado watu walikuwa wanastaajabia hayo yote aliyokuwa akiyafanya Isa, yeye akawaambia wanafunzi wake: 44“Sikilizeni kwa makini haya nitakayowaambia sasa: Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutiwa mikononi mwa watu.” 45Lakini wao hawakuelewa alimaanisha nini. Maana ya maneno hayo ilifichika kwao, hivyo hawakuyaelewa, nao wakaogopa kumuuliza maana yake.
Ni nani atakayekuwa mkuu
(Mathayo 18:1-5; Marko 9:33-37; Luka 22:24-30)
46Kukazuka mabishano miongoni mwa wanafunzi kuhusu ni nani miongoni mwao atakayekuwa mkuu kuliko wote. 47Lakini Isa akayatambua mawazo yao, naye akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha kando yake. 48Kisha akawaambia, “Yeyote amkaribishaye mtoto huyu mdogo kwa Jina langu, anikaribisha mimi, na yeyote atakayenikaribisha mimi, atakuwa amemkaribisha yeye aliyenituma. Kwa maana yeye aliye mdogo miongoni mwenu, ndiye aliye mkuu kuliko wote.”
Yeyote asiye kinyume nasi yuko upande wetu
(Marko 9:38-41)
49Yohana akasema, “Bwana, tumemwona mtu akitoa pepo wachafu kwa jina lako, nasi tukamzuia, kwa sababu yeye si mmoja wetu.”
50Isa akasema, “Msimzuie, kwa sababu yeyote ambaye si kinyume nanyi, yu upande wenu.”
Safari ya Isa kwenda Yerusalemu
(Luka 9:51–19:44)
Isa akataliwa Samaria
51Wakati ulipokaribia wa yeye kuchukuliwa mbinguni, alikaza uso wake kwenda Yerusalemu. 52Akatuma watu wamtangulie, nao wakaenda katika kijiji kimoja cha Samaria kumwandalia kila kitu; 53lakini watu wa kijiji kile hawakumkaribisha kwa sababu alikuwa anaenda zake Yerusalemu. 54Wanafunzi wake, yaani Yakobo na Yohana, walipoona hayo, wakasema: “Bwana Isa, unataka tuagize moto kutoka mbinguni ili uwaangamize?” 55Isa akageuka na kuwakemea. 56Naye Isa na wanafunzi wake wakaenda kijiji kingine.
Gharama ya kumfuata Isa
(Mathayo 8:19-22)
57Walipokuwa njiani wakienda, mtu mmoja akamwambia Isa, “Nitakufuata popote utakakoenda.”
58Isa akamjibu, “Mbweha wana mapango, nao ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”
59Isa akamwambia mtu mwingine, “Nifuate.”
Mtu huyo akamjibu, “Bwana#9:59 Wale ambao hawakumfahamu Isa kuwa Masihi walimwita “Bwana” kwa heshima ya kawaida., niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.”
60Isa akamwambia, “Waache wafu wawazike wafu wao, bali wewe nenda ukautangaze ufalme wa Mungu.”
61Mtu mwingine akamwambia, “Bwana, nitakufuata lakini naomba kwanza nikawaage jamaa zangu.”
62Isa akamwambia, “Mtu yeyote ashikaye jembe kulima kisha akatazama nyuma hafai kwa ufalme wa Mungu.”