UTANGULIZI
Injili ilivyoandikwa na Luka ni sehemu ya kwanza ya maandishi aliyoandika Luka, sehemu ya pili ikiwa ni kitabu cha Matendo ya Mitume. Luka anatamka dhahiri kwamba jukumu lake ni kuwapatia wasomaji wake mambo aliyofundisha Yesu na kutenda, au Habari Njema, ambayo imeandikwa kwa mpango, hatua kwa hatua, kuanzia kuzaliwa kwake Yohane Mbatizaji mpaka Yesu alipochukuliwa mbinguni na mitume wakaanza kueneza hizo Habari njema kama tunavyosimuliwa katika kitabu cha pili. Hatujui mengi kuhusu Luka binafsi ila yaonekana alikuwa mtu aliyeelimika, daktari, na ambaye kwa muda mfupi alikuwa mwenzake Paulo katika safari zao za kuhubiri Habari Njema (ling Kol 4:14; 2 Tim 4:11 na Fil 24).
Injili hii huenda iliandikwa yapata mwaka 80 B.K. Luka, katika kuiandika, anamtaja mtu fulani, Theofilo ambaye alikuwa amepata habari za Yesu wa Nazareti. Luka anataka kumwandikia tena habari hizo kwa mpango.
Ili kuonesha kwamba matukio hayo ni ya kihistoria, Luka ni mwangalifu sana katika kuyawekea tarehe kulingana na matukio mengine ya nyakati hizo.
Injili yenyewe inaeleza kinaganaga matukio muhimu katika maisha ya Yesu Kristo. Luka anaanza kwa kutufahamisha kuwa Yesu ndiye Mkombozi wa Israeli na wa watu wote. Jambo moja la kipekee kuhusu Injili ya Luka ni huduma ya Yesu kwa watu wote. Jambo hili ni wazi tukiangalia jinsi Luka anavyoorodhesha ukoo wa Yesu kinyumenyume kuanzia na Yesu mwenyewe hadi Adamu, babu wa kwanza wa binadamu wote, ili kuonesha kwamba hata wasio Waisraeli wana haki ya kupokea wokovu wa Mungu.
Mtazamo huu wa kuwajali watu wote unajitokeza wazi kutokana na jinsi Yesu anavyowajali watu wasiobahatika na wasioheshimiwa kijamii na kidini. Hawa ni pamoja na maskini, wahitaji, walemavu, wajane, wahalifu na wenye dhambi. Ni muhimu kutambua kwamba Yesu anatangaza kwamba kuwahubiria maskini Habari Njema ni mojawapo ya sifa zake maalumu au kitambulisho kama Masiha (Luka 4:18-19). Kufuatana na msimamo wake huu wa kuwajali maskini, Injili hii inazo sehemu kadhaa zinazowapa watu tahadhari juu ya utajiri, na mkazo juu ya utekelezaji wa haki katika jamii. Aghalabu watu haohao waliotengwa na jamii na kutoshirikishwa kidini ndio ambao Yesu anawaahidi kuwakweza katika ufalme wake.
Yapo mambo mengine pia yanayoitofautisha Injili hii. Injili yote inatilia sana mkazo sala, hasa wakati wa matukio makuu katika huduma ya Yesu, na habari juu ya Roho Mtakatifu, na toba.
Tunafahamu pia kwamba Injili ya Luka kama vile ile ya Mathayo, ilitumia kama mwongozo, maandishi ya Injili ya Marko. Lakini zipo pia habari fulanifulani katika Injili hii ambazo hazipatikani katika Injili nyingine: Habari hizo ni pamoja na hali ilivyokuwa Kristo alipozaliwa, tenzi za sifa, kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji, wachungaji kumwabudu mtoto Yesu, mtoto Yesu hekaluni. Pia kuna habari za miujiza kama ule wa kuvua samaki wengi, kufufuliwa mtoto wa mama mjane huko Naini, kutakaswa wakoma kumi, na baadhi ya mifano kama ule wa Msamaria Mwema, mtoto mpotevu, tajiri na Lazaro, na Farisayo na mtozaushuru. Kunazo pia baadhi ya simulizi kama habari juu ya Zakayo, safari ya kwenda Emau, ambayo yaonesha kuwa jambo muhimu au lengo muhimu siyo tu kumtambua Yesu aliyefufuka katika kumega mkate, bali, “… kusadiki yote yaliyonenwa na manabii” (24:25) juu ya Yesu Kristo. Jambo lingine linalojitokeza katika Injili hii ni hali ya furaha, hasa katika kutangaza kuja na kupaa kwake Yesu. Habari za kukua na kuenea kwa imani ya Kikristo baada ya kupaa kwake Yesu zinaelezwa na mwandishi huyuhuyu katika kitabu cha Matendo ya Mitume.