Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 19

19
1Basi ndipo Pilato alipomtwaa Yesu, akampiga mijeledi. 2Nao askari wakasokota taji la miiba, wakamtia kichwani, wakamvika vazi la zambarau. 3#Yn 18:22 Wakawa wakimwendea, wakisema, Salamu! Mfalme wa Wayahudi! Wakampiga makofi. 4Kisha Pilato akatokea tena nje, akawaambia, Mtu huyu namleta nje kwenu, mpate kufahamu ya kuwa mimi sioni hatia yoyote kwake. 5Ndipo Yesu alipotoka nje, naye amevaa lile taji la miiba, na lile vazi la zambarau. Pilato akawaambia, Tazama, mtu huyu! 6Basi wale wakuu wa makuhani na watumishi wao walipomwona, walipiga kelele wakisema, Msulubishe! Msulubishe! Pilato akawaambia, Mtwaeni ninyi basi, mkamsulubishe; kwa maana mimi sioni hatia kwake. 7#Yn 5:18; 10:33; Law 24:16 Wayahudi wakamjibu, Sisi tunayo sheria, na kwa sheria hiyo amestahili kufa, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu.
8Basi Pilato aliposikia neno hilo, akazidi kuogopa. 9Akaingia tena ndani ya ile Praitorio, akamwambia Yesu, Wewe umetoka wapi? Lakini Yesu hakumpa jibu lolote. 10Basi Pilato akamwambia, Husemi nami? Hujui ya kuwa mimi nina mamlaka ya kukufungua, nami nina mamlaka ya kukusulubisha? 11#Yn 10:18; Mdo 2:23 Yesu akamjibu, Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu; kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako ana dhambi iliyo kubwa zaidi. 12#Mdo 17:7 Na tangu hapo Pilato akatafuta kumfungua; lakini Wayahudi wakapiga makelele wakisema, Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu ajifanyaye kuwa mfalme humfitini Kaisari. 13Basi Pilato, aliposikia maneno hayo, akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu, mahali paitwapo Sakafu ya Mawe, au kwa Kiebrania, Gabatha. 14Nayo ilikuwa Maandalio ya Pasaka, yapata saa sita. Akawaambia Wayahudi, Tazama, Mfalme wenu! 15#Yn 19:6 Basi wale wakapiga kelele, Mwondoshe! Mwondoshe! Msulubishe! Pilato akawaambia, Je! Nimsulubishe mfalme wenu! Wakuu wa makuhani wakamjibu, Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.
Kusulubiwa kwa Yesu
16 # Mt 27:31-50; Mk 15:20-37; Lk 23:26-46 Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulubiwe; nao wakampokea Yesu. 17Akatoka, huku akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha. 18Wakamsulubisha huko, na wengine wawili pamoja naye, mmoja huku na mmoja huku, na Yesu katikati. 19Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI. 20Basi anwani hiyo waliisoma wengi katika Wayahudi; maana mahali pale aliposulubiwa Yesu palikuwa karibu na mji; nayo iliandikwa kwa Kiebrania, na Kirumi, na Kigiriki. 21Basi wakuu wa makuhani na Wayahudi wakamwambia Pilato, Usiandike, Mfalme wa Wayahudi; bali ya kwamba yule alisema, Mimi ni mfalme wa Wayahudi. 22Pilato akajibu, Niliyoandika nimeyaandika.
23Nao askari walipomsulubisha Yesu, waliyatwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kwa kila askari fungu lake; na kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa imefumwa yote pia tangu juu. 24#Zab 22:18 Basi wakaambiana, Tusiipasue, lakini tuipigie kura, iwe ya nani. Ili litimie andiko lile linenalo,
Waligawanya nguo zangu,
Na vazi langu wakalipigia kura.
Basi ndivyo walivyofanya wale askari.
25Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene. 26#Yn 13:23 Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. 27Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.
28 # Zab 22:15; 69:21; Yn 13:3; 18:4 Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, Naona kiu. 29#Zab 69:21 Kulikuwako huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani. 30Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, Imekwisha. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.
Yesu achomwa mkuki ubavuni
31 # Kum 21:23 Basi Wayahudi, kwa sababu ni Maandalio, miili isikae juu ya misalaba siku ya sabato, (maana sabato ile ilikuwa siku kubwa), walimwomba Pilato miguu yao ivunjwe, wakaondolewe. 32Basi askari wakaenda, wakamvunja miguu wa kwanza, na wa pili, aliyesulubiwa pamoja naye. 33Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu; 34lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji. 35Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya kuwa anasema kweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki. 36#Kut 12:48; Hes 9:12; Zab 34:20 Kwa maana hayo yalitukia ili andiko litimie,
Hapana mfupa wake utakaovunjwa.
37 # Zek 12:10; Ufu 1:7 Na tena andiko lingine lanena,
Watamtazama yeye waliyemchoma.
Kuzikwa kwa Yesu
38 # Mt 27:57-61; Mk 15:42-47; Lk 23:50-55 Hata baada ya hayo Yusufu wa Arimathaya, naye ni mwanafunzi wa Yesu, (lakini kwa siri, kwa hofu ya Wayahudi), alimwomba Pilato ruhusa ili auondoe mwili wake Yesu. Na Pilato akampa ruhusa. Basi akaenda, akauondoa mwili wake. 39#Yn 3:1-2; Mt 2:11 Akaenda Nikodemo naye, (yule aliyemwendea usiku hapo kwanza), akaleta mchanganyiko wa manemane na uudi, yapata ratili mia. 40Basi wakautwaa mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika. 41Na pale pale aliposulubiwa palikuwa na bustani; na ndani ya bustani mna kaburi jipya, ambalo hajatiwa bado mtu yeyote ndani yake. 42Humo basi, kwa sababu ya Maandalio ya Wayahudi, wakamweka Yesu; maana lile kaburi lilikuwa karibu.

Iliyochaguliwa sasa

Yohana 19: RSUVDC

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia