1 Mose 16
16
Sarai anampa Aburamu kijakazi wake Hagari kuwa mkewe.
1Sarai, mkewe Aburamu, hakumzalia mwana. Naye alikuwa na kijakazi wa Kimisri, jina lake Hagari. 2Kwa hiyo akamwambia Aburamu: Unaona, ya kuwa Bwana amenifunga, nisizae; sasa ingia kwa kijakazi wangu! Labda nitapata mlango kwake yeye. Aburamu akayaitikia, Sarai aliyoyasemaa.#1 Mose 30:3,9; 1 Kor. 7:2. 3Kisha Sari, mkewe Aburamu, akamchukua Hagari, kijakazi wake wa Kimisri, akampa mumewe Aburamu kuwa mkewe, Aburamu naye alikuwa amekwisha kukaa miaka kumi katika nchi ya Kanaani. 4Alipoingia kwake Hagari, huyu akapata mimba; naye alipojiona kuwa mwenye mimba akambeua bibi yake, awe mdogo machoni pake. 5Ndipo, Sarai alipomwambia Aburamu: Mabaya ninayofanyiziwa na yakujie wewe! Mimi nimemweka kijakazi wangu kifuani pako; naye alipojiona kuwa mwenye mimba hunibeua, niwe mdogo machoni pake. Bwana na atuamulie mimi na wewe! 6Naye Aburamu akamwambia Sarai: Tazama, kijakazi wako yumo mkononi mwako! Mfanyizie yaliyo mema machoni pako! Lakini Sarai alipomnyenyekeza, akatoroka usoni pake.
Hagari anamzaa Isimaeli.
7Malaika wa Bwana akamwona nyikani penye kisima cha maji, ndicho kisima kilichoko katika njia ya Suri. 8Akasema: Hagari, kijakazi wa Sarai, unatoka wapi? Tena unakwenda wapi? Akasema: Nimetoroka, nitoke usoni pake bibi yangu Sarai. 9Ndipo, malaika wa Bwana alipomwambia: Rudi kwa bibi yako na kuunyenyekea mkono wake! 10Malaika wa Bwana akamwambia tena: Wao wa uzao wako nitawafanya kuwa wengi, wasihesabike kwa wingi.#1 Mose 17:20. 11Malaika wa Bwana akaendelea kumwambia: Ninakuona kuwa mwenye mimba. Mwana, utakayemzaa, mwite jina lake Isimaeli (Mungu husikia), kwa kuwa Bwana amekusikia, ulipomlalamikia kwa kuteseka. 12Naye atakuwa mwenye ukali kama punda wa porini, mkono wake utawapingia watu wote, nayo mikono yao wote itampingia yeye, naye atakaa mbele yao ndugu zake wote.#1 Mose 25:18. 13Ndipo, alipomwita Bwana aliyesema naye jina lake: Wewe Mungu unaniona, kwani alisema: Kumbe nami nimemwona, aliponitazama. 14Kwa hiyo kile kisima watu hukiita Kisima cha Mwenye Uzima Anionaye, nacho kiko katikati ya Kadesi na Beredi.#1 Mose 24:62; 25:11. 15Kisha Hagari akamzalia Aburamu mtoto mume, naye Aburamu akamwita huyu mwana, Hagari aliyemzaa, jina lake Isimaeli. 16Naye Aburamu alikuwa mwenye miaka 86, Hagari alipomzalia Aburamu huyu Isimaeli.
Iliyochaguliwa sasa
1 Mose 16: SRB37
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.